WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wazazi wahakikishe
vijana wao wanakwenda kusoma kwenye shule za sekondari kwani bila elimu
hawawezi kufika mbali.
“Wazazi wenzangu hakikisheni vijana wenu wanaenda shule.
Hatuwezi kufika mbali kama vijana wetu hawaendi shule. Tunajenga shule kila
mahali, tunataka maeneo yote yawe na shule,” alisema.
Waziri Mkuu Majaliwa ambaye pia ni Mbunge wa Ruangwa alitoa
kauli hiyo jana (Alhamisi, Agosti 22, 2024) wakati akizungumza na wakazi wa
kijiji cha Mtondo, Kata ya Nambiranje, Ruangwa mkoani Lindi.
Akielezea hatua iliyofikiwa kutokana na juhudi za Serikali
ya awamu ya sita, Waziri Mkuu alisema Wilaya ya Ruangwa imepiga hatua kwenye
sekta za elimu, maji na afya ikilinganishwa na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma.
Alisema wilaya hiyo ina shule tatu za wasichana pekee ambazo
ni Liuguru, Ruangwa Girls na Lucas Malia. “Vilevile tumefanikiwa kujenga shule
za sekondari zenye kidato cha tano na sita ambazo ni Ruangwa, Mbekenyera,
Nkowe, Lucas Malia na Hawa Mchopa. Shule ya sita ya Mandawa itakamilika hivi
karibuni,” alisisitiza.
Akielezea utekelezaji kwenye sekta ya maji, Waziri Mkuu
alisema vijiji vyote 90 vya wilaya vilichimbiwa maji kupitia taasisi ya GAIN
lakini kwa sasa hayatoshi. Hata hivyo, alitumia fursa hiyo kuwajulisha kwamba
Serikali imetoa sh. bilioni 49 kwa ajili ya ujenzi wa mradi wa maji kutoka
Nyangao ambao utavinufaisha vijiji 34 vya wilaya ya Ruangwa na vijiji 29 vya
wilaya ya Nachingwea.
Kuhusu umeme, alisema kwamba laini zimeshaenda kwenye kila
kijiji na kwamba Serikali hivi sasa inashughulika kuweka umeme kwenye ngazi ya
vitongoji. “Leo hii hakuna kijiji kisichokuwa na umeme.”
Kuhusu barabara, alisema kuna changamoto ya barabara kufika
katika kijiji cha Mtondo ambayo tayari iko kwenye mpango wa ujenzi. “Kuna
barabara ya kutoka Mandawa Chini hadi hapa, Nanjalu hadi hapa, Nambiranje hadi
hapa na kutoka Namiyenje hadi hapa.”
Mapema, Diwani wa Kata ya Nambiranje, Mossa Mohammed Mtejela
alimuomba Waziri Mkuu awasaidie ili waongezewe fedha za ujenzi wa barabara ya
kutoka Mtondo hadi Mkaranga Sekondari yenye urefu wa kilometa saba kwa sababu
kuna daraja linapaswa kujengwa na fedha iliyotengwa ni sh. milioni 300 tu.
“Tunaomba utusaidie ili tuongezewe fedha za ujenzi wa
barabara ya Mtondo hadi Mkaranga Sekondari na daraja la mto Moha kwenye kijiji
cha Mkaranga. Shilingi milioni 300 zilizotolewa haziwezi kutosha,” alisema.
Pia aliomba wajengewe bweni la wavulana kwenye sekondari ya
Nambiranje kwa sababu kuna baadhi ya wanafunzi wanatembea km.7.5 kutoka Mtondo
na wengine km. 16 kutoka Nanjalu. “Tunaomba tujengewe bweni ili kuwasaidia
watoto wetu lakini pia kupunguza utoro wa rejareja,” alisema.
Shule hiyo ya kata tayari ina bweni moja la wasichana lenye
uwezo wa kuchukua wanafunzi 80.
Waziri Mkuu anaendelea na ziara jimboni kwake.
0 Maoni