Wananchi wa Kijiji cha Mwajiji kilichopo Kata ya Lyabusalu,
Wilaya ya Shinyanga Vijijini mkoani Shinyanga wametoa pongezi kwa Wakala ya
Barabara za Vijijini na Mijini Tanzania (TARURA) kwa ujenzi wa barabara ya
Mwajiji yenye urefu wa KM 5.
Pongezi hizo zimetolewa kijijini hapo, ambapo wananchi
walieleza changamoto walizokuwa wakizipata kabla ya ujenzi wa barabara hiyo,
ikiwemo wanawake kujifungulia njiani kutokana na barabara hiyo kuwa na tope
wakati wa masika.
“Wakati wa masika tulikuwa tunapata shida sana kupita kwenye
barabara hii, kutokana na barabara kujaa tope, hivyo vyombo vya usafiri
kushindwa kupita, na wakati mwingine vilikuwa vikitumia muda mrefu kutoka eneo
moja kwenda eneo lingine,” amesema Mwenyekiti wa Kijiji cha Mwajiji, Maligisa
Mbuya.
Ameendelea kusema kuwa, baadhi ya wakina mama walijifungulia
njiani kutokana na adha ya barabara hiyo, ambapo walikuwa wakitumia muda mrefu
njiani, na kucheleweshwa kufika katika kituo cha afya.
“Kwa sasa barabara inapitika vizuri, na imefika mpaka kituo
cha afya, hivyo tatizo la wakina mama kujifungulia njiani halitakuwepo tena,
tunaishukuru serikali kwa kutukumbuka wananchi wa Mwajiji,” amesema mwenyekiti
huyo.
Aidha, amesema kuwa, barabara hiyo itafungua uchumi wa
kijiji hicho, kwani wakazi wengi wa eneo hilo ni wakulima, hivyo uwepo wa
barabara utawarahisishia usafirishaji wa mazao yao kutoka mashambani mpaka
kwenye masoko.
Kwa upande wake Meneja wa TARURA Mkoa wa Shinyanga, Mhandisi
Avith Theodory amesema katika mkoa wa Shinyanga TARURA ina hudumia mtandao
wa barabara wenye Km. 5,220, ambazo kati
ya hizo Km. 40.9 ni barabara za lami, Km. zaidi ya 2,000 ni barabara za
changarawe na Km. zaidi ya 3,100 ni barabara za udongo.
Mhandisi Theodory amempongeza Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuipatia TARURA fedha
ili kuweza kutekeleza majukumu yake.
“Miaka mitatu nyuma, TARURA ilikuwa na bajeti ya takribani bilioni 7.2, lakini kwa kipindi hiki cha miaka mitatu, bajeti imeongezeka mpaka kufikia bilioni 18, ambazo zimefanya maendeleo makubwa ya miundombinu ya barabara katika mkoa wa Shinyanga,” amesema Mhandisi Theodory.
0 Maoni