WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Oktoba
16, 2024 amemwakilisha Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan katika maziko
ya Mzee Jeremiah Kusiluka ambaye ni Baba mzazi wa Katibu Mkuu Kiongozi Balozi
Dkt. Moses Kusiluka yaliyofanyika katika kijiji cha Madihani, Makete mkoani
Njombe.
Akitoa salamu za Mheshimiwa Rais Dkt.
Samia, Waziri Mkuu amesema Mheshimiwa
Rais Dkt. Samia ametoa wito kwa wanafamilia, ndugu na waombolezaji wawe
watulivu katika kipindi hiki kigumu za msiba huo na waendelee kumuombea
marehemu Mzee Jeremiah ili Mwenyezi Mungu amlaze mahali pema peponi.
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa ametoa wito
kwa wanafamilia, ndugu na waombolezaji kuyaenzi mema yote aliyoyafanya marehemu
kipindi cha uhai wake. “Tuenzi yale yote mema aliyoyafanya mzee wetu Jeremiah
wakati wa uhai wake, tukifanya hivyo tutakuwa tumetenda haki. ”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu
amesema kuwa Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango na Rais wa Zanzibar na
Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Mwinyi wanatoa pole kwa
wanafamilia, ndugu na waombolezaji kutokana na msiba huo.
Akizungumza kwa Niaba ya Familia,
Prof. Lughano Kusiluka ametoa shukrani kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na
Serikali kwa ujumla kwa kushiriki wake katika kumuaga Mzee Jeremiah. “Asanteni
kwa kuja kushiriki nasi, tunawashukuru sana kwa kutuunga mkono kuja kushiriki
nasi katika kumuaga mzee wetu, heshima hii ni kubwa na haielezeki. ”
Aliongeza kuwa Mzee Jeremiah alikuwa
ni Baba imara na mwenye msimamo. “Mara zote alitusisitiza lazima tuheshimu watu
tufanye kazi ili tuweze kuishi na alitukumbusha kuwa hapa katika kijiji cha
Madihani, Kipahalo ni nyumbani kwetu, ” alisema.
Kwa Upande wake Katibu Mkuu Kiongozi
Balozi Dkt. Moses Kusiluka amesema kuwa Marehemu Mzee Jeremiah alikuwa ni
mpenda maendeleo na watoto wake wote wamekuwa wakienzi msimamo huo. “Pamoja na
kuwa mpenda maendeleo pia baba alikuwa mchaMungu na ameondoka akiwa mchaMungu.
”
Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha
Mapinduzi Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi amesema kutokana na historia ya mzee
Jeremiah hasa kwenye malezi ya watoto wake inapaswa kusherehekea maisha yake
kwa kuwa anakuwa shujaa wa Makete na Tanzania kwa ujumla. “Mafanikio ya watoto
wake katika utumishi wa umma hayana kificho. ”
Viongozi walioshiriki msiba huo ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) William Lukuvi,
Mkuu wa Mkoa wa Njombe Anthony Mtaka, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Juma Homera na Mkuu
wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule.
Wengine ni Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri
Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Dkt. Jim Yonaz, Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhandisi Antony Sanga, Katibu Mkuu Wizara ya Afya
Dkt. John Jingu, Msajili wa Hazina Nehemia Kyando Mchechu.
0 Maoni