Serikali kupitia Wizara ya Madini
inarudisha minada ya ndani ya madini ya vito itakayofanyika katika maeneo ya
uzalishaji hususan Mirerani, Mahenge, Tunduru, Dar es salaam, Arusha na Tanga
na kimataifa itafanyika mji wa Bangkok na Jaipur nchini Thailand.
Hayo yamesemwa leo Oktoba 16, 2024 na
Waziri wa Madini Mhe. Anthony Mavunde wakati akijibu hoja mbalimbali
zilizoibuliwa na wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Nishati na Madini
jijini Dodoma.
Waziri Mavunde amesema kuwa baada ya
taratibu za marekebisho ya kisheria kukamilika juu ya uendeshaji wa minada hiyo
wanatarajia ndani ya muda mfupi ujao kuanza taraibu za kuweka miundombinu ya
kuanza minada ya ndani.
Waziri Mavunde amefafanua kuwa,
uendeshaji wa maonesho na minada ya kimataifa nchini ni fursa muhimu ya
kutangaza madini ya vito yanayozalishwa hususan kwenye masoko ya kimataifa
ambayo ni njia mojawapo ya kuwafikisha watanzania katika masoko ya uhakika na
upatikanaji wa bei nzuri na stahiki.
Waziri Mavunde ameieleza Kamati ya
Nishati na Madini kuwa, Mpango wa kurejesha minada ya madini ya vito ni
utekelezaji wa maagizo yaliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Dkt. Samia Suluhu Hassan wakati wa ufunguzi wa kiwanda cha kusafisha
dhahabu cha jijini Mwanza tarehe 13 Juni, 2024.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Madini
Dkt. Steven Kiruswa amesema, kwa sasa wataalam wa Wizara ya Madini wamepata
uzoefu mkubwa katika minada na maonesho ya kimataifa baada ya kujifunza namna
biashara za kimataifa zinavyofanyika pamoja na matumizi ya teknolojia ya kisasa
kwenye mnyororo mzima wa thamani madini katika nchi mbalimbali ikiwemo Marekani
, India , Afrika Kusini na Thailand.
Awali, akiwasilisha taarifa kuhusu
uboreshaji na utekelezaji wa Kanuni za Usimamizi wa Masoko na vituo, minada ya
ndani na kimataifa ya madini ya vito kwa Kamati hiyo, Kaimu Mtendaji Tume ya
Madini Mhandisi Ramadhani Lwamo amesema kuwa, minada hiyo itaendeshwa na Tume
ya Madini kwa kushirikiana na Soko la Bidhaa la Tanzania (TMX) kupitia mfumo wa
mauzo wa kielektroniki ambapo usimamizi
utahusisha shughuli za uthaminishaji na upangaji wa madini ili kuweza kupata
bei nzuri kulingana na madini husika,akisisitiza kwamba lengo kuu ni kuifanya
Tanzania kuwa kitovu cha biashara ya madini ya vito na usonara barani Afrika.
Mhandisi Lwamo ameongeza kuwa, minada
ya vito itaifungamanisha Sekta ya Madini na Sekta nyingine za kiuchumi ikiwemo
Utalii na biashara katika kipindi husika ikiwa ni pamoja na kuliingizia taifa
fedha za kigeni.
Pamoja na mambo mengine, Mwenyekiti wa
Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini Dkt. David Mathayo ameendelea kumpongeza
Waziri wa Madini na wasaidizi wake kwa kazi nzuri ya kuisongesha Sekta ya
Madini katika ngazi ya kimataifa inayoleta tija katika uchumi wa nchi na hasa
katika mkakati wa kurudisha hadhi na thamani ya madini ya vito yakiwemo madini
ya Tanzanite ambayo ni madini yanayopatikana Tanzania peke yake.
0 Maoni