Kundi la watalii zaidi ya 25 kutoka nchini India leo
wametembelea Msitu wa Hifadhi wa Rau uliopo umbali wa kilomita 3 kutoka Moshi
Mjini kwa ajili ya kutalii na kuona jinsi shughuli za uhifadhi wa misitu
zinavyoenda sambamba na huduma zitokanazo na misitu ikiwemo Utalii.
Watalii hawa ambao wapo kwenye maandalizi ya kupanda Mlima
Kilimanjaro wametumia ziara ya kutembelea Hifadhi ya Rau kama sehemu ya
kujiandaa na hali ya hewa kabla ya kupanda Mlima.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo Sandeep Vijaykumar Shah
Mwanzilishi na Mkurugenzi wa Reroute Intergrated Fitness ambayo ni taasisi
iliyoratibu safari hii anasema lengo la safari hii ni kuhamasisha shughuli za
uhifadhi wa misitu na wanyamapori na kuhakikisha wanapaza sauti ili kuongeza
jitihada za uhifadhi na kukabiliana na Mabadiliko ya Tabianchi.
"Kwa hali ya sasa ya ongezeko la joto duniani, ni
muhimu zaidi kuliko wakati wowote mwingine kutangaza umuhimu wa kuhifadhi
misitu kwani ina jukumu muhimu katika kupunguza athari zitokanazo na mabadiriko
ya tabianchi na kutoa makazi kwa aina nyingi za wanyama," anasema.
Akizungumza kwa niaba ya Mhifadhi wa Msitu wa Hifadhi ya
Rau, Mhifadhi Zayana Mrisho anasema msitu huo una vivutio vingi ikiwemo mimea
pamoja na miti ya asili ambayo haipatikana katika maeneo mengine, ikiwemo Mti
wa Mvule ambayo unazaidi ya miaka 200 na ni mrefu kuliko yote barani Afrika.
Aliongeza kuwa utalii mkubwa unaofanyika katika msitu huo ni
Utalii wa baiskeli, ibada, tafiti na masomo, picha, nyuki na kuangalia
madhari ya misitu, ndege na wanyama wanaopatikana ndani ya hifadhi.
Aidha, alisema kuwa Wakala wa Huduma za
Misitu Tanzania (TFS), Wilaya ya Moshi, Mkoa wa Kilimanjaro,
wameendelea kuutangaza utalii wa ndani ambapo sasa wameweka nguvu kubwa katika
hifadhi ya Msitu huo kwa kampeni ya Tukacharu Rau-Mtoko Nyika ambayo
wataizindua rasmi Jumanne Agosti 13, 2024 katika msitu huo.
Ziara hii imehusisha vijana wadogo chini ya miaka 15 hadi wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.
0 Maoni