Kigogo Taasisi ya Mwalimu Nyerere ajitosa ubunge Afrika Mashariki

 

Makamu Mwenyekiti wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere Mkoa wa Kilimanjaro, Grace Saulo Mali, amechukua fomu ya kuomba ridhaa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuwania ubunge wa Bunge la Afrika Mashariki (EALA).

Kada huyo wa CCM ambaye kitaaluma ni mwalimu, amechukua fomu hiyo  mapema leo katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya Chama, Mtaa wa Lumumba, jijini Dar es Salaam.

Akizungungumza na waandishi wa habari baada ya kuchukua fomu hiyo Grace amesema ana dhamira ya dhati ya kuwania kiti hicho kilicho achwa wazi na aliyekuwa Mbunge wa Bunge la Afrika Mashariki, Dk.Shogo Mlozi, aliyefariki dunia Juni mwaka huu.

Grace amemshukuru Mwenyekiti wa CCM Rais Dk.Samia Suluhu Hassan na Chama kwa kuweka utaratibu mzuri wa kuwania nafasi hiyo.

Amesema, kipaumbele chake kikubwa atakapo pata nafasi hiyo ya kuliwakilisha taifa katika Bunge la Afrika Mashariki ni elimu.

“Pia kuwasaidia vijana waliosoma lakini hawana ajira kwa kuwaunganisha na fursa,”amesema.

 Amewataka watanzania kumuunga mkono Rais Dk. Samia katika sekta mbalimbali alizowekeza.

CCM jana imeanza kutoa fomu hizo nchini kote.

Chapisha Maoni

0 Maoni