Dk. Nchimbi akutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa China

 

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Idara ya Mambo ya Nje wa Chama cha Kikomunisti cha China (CPC), Ndugu Liu Jianchao, ambaye amesema kuwa CPC na Serikali yake, wanatambua juhudi kubwa za kuleta maendeleo zinazofanywa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo na Katibu wa NEC Siasa na Uhusiano wa Kimataifa Rabia Hamid,  Ndugu Jianchao amesema kuwa chini ya uongozi wa Mhe. Dkt. Samia, Tanzania imekuwa na mabadiliko makubwa, yanayoonekana katika nyanja zote za viashiria vya ukuaji uchumi.

Katika mazungumzo hayo yaliyofanyika Makao Makuu ya Ofisi za Idara ya Mambo ya Nje ya CPC (IDCPC), jijini Beijing, China, Jumatatu, Agosti 26, 2024, Balozi Nchimbi, pamoja na kufikisha salamu za Mwenyekiti wa CCM na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia, amesema kuwa CCM, Serikali zake mbili na Tanzania kwa ujumla wanaichukulia China, ni mojawapo ya mifano ya kuigwa.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa chini ya uongozi wa Mhe. Rais Xi Jinping, CPC imeweza kuiongoza China kupiga hatua za maendeleo makubwa kwa kipindi cha miaka 10 iliyopita.

Kupitia mazungumzo hayo, Balozi Nchimbi na Ndugu Jianchao, wamerejea msingi imara wa uhusiano wa vyama vyao na nchi hizi mbili, tangu wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere na Mwenyekiti Mao Zedong na wamekubaliana umuhimu wa kuendelea kuimarisha udugu huo wa kirafiki, kwa ajili ya manufaa ya Tanzania na China.

Mkutano huo wa Balozi Nchimbi na Ndugu Jianchao ni sehemu ya ratiba ya ziara ya Ujumbe wa Viongozi wa CCM nchini China, iliyoanza Agosti 24, 2024, inayolenga kuendeleza na kuimarisha zaidi urafiki wa kihistoria kati ya vyama vya CCM na CPC na uhusiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China, ambao umedumu kwa miongo sita sasa.



Chapisha Maoni

0 Maoni