Wananchi wa Kata ya Bugwena kusahau adha ya maji

 

Wananchi wa Kata ya Bugwema iliyopo katika jimbo la Musoma Vijijini wilayani Musoma wameishukuru Serikali pamoja na mbunge wao Prof. Sospeter Muhongo kwa kufanikisha kuanza kwa zoezi la uchimbaji visima vitano.

Wananchi hao wamesema visima hivyo vya maji vitasaidia kuondokana na adha ya maji ambayo imekuwa ikiwasumbua kwa muda mrefu na kuchangia kudhorotesha shughuli zingine za kijamii na kiuchumi.

“Kutokana na eneo letu kuwa na ukame tumeteseka sana kupata maji safi na salama, tulikuwa tunatafuta maji kwenye matope na maji hayo ni machafu yanatupatia maradhi ya kichocho, lakini sasa tunawamshukuru sana Rais Samia Suluhu Hassan na mbunge wetu,” walisema wananchi hao.

Hapo jana Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt Khalfany Haule alipokea na kushuhudia gari lenye mtambo wa uchimbaji wa visima virefu vya maji ukianza kazi kwenye Kata ya Bugwema jimbo la usoma Vijijini.

Meneja wa RUWASA wa Wilaya ya Musoma, Injinia Edward Sironga ameeleza kuwa maji kutoka kwenye visima hivyo vitano virefu vinavyochimbwa yatasambazwa kwa mabomba ndani ya vijiji venye visima hivyo.

“Kazi hii ni ya mradi wa visima 900 nchi nzima, ambapo kwa Jimbo la Musoma sisi tulichagua mradi huu kuchimba visima vitano katika Kata ya Bugwema kutokana na eneo hili kukabiliwa na ukame,” alisema Bw. Sironga.

Imeelezwa kuwa mbali ya upatikanaji wa maji kutoka visima virefu, vijiji vyetu vyote 68 vina miradi ya kusambaziwa maji ya bomba kutoka Ziwa Victoria. Miradi hii ipo kwenye hatua mbalimbali za utekelezaji wake.



Chapisha Maoni

0 Maoni