Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limekemea tabia iliyoanza kuibuka ya baadhi ya watu kutoa taarifa zisizo sahihi kwenye mitandao ya kijamii kuhusu kuuawa au kutekwa kwa watoto katika maeneo mbalimbali nchini.
Taarifa iliyotolewa leo na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile imesema Jukwaa la Wahariri Tanzania linafuatilia kwa karibu tabia iliyoibuka hivi sasa ya baadhi ya watu kutoa taarifa zisizo sahihi kuhusu kuuawa au kutekwa kwa watoto katika maeneo mbalimbali nchini.
“Yamekuwapo matukio kadhaa ya taarifa za aina hii katika maeneo ya Jiji la Dar es Salaam, huko Kigamboni, Mbagala na Kipawa, ambayo yameleta taharuki kubwa hadi wazazi wakafuatawatoto shule, lakini baadaye ikathibitika kuwa siyo kweli,” imesema taarifa hiyo na kuongeza, “Tabia hii ya kupokea na kusambaza taarifa ambazo hazina uhakika au ukweli, husababisha taharuki, usumbufu, na mshtuko kwa wazazi, walezi, watoto, na wananchi kwa ujumla.”
TEF imewaomba Watanzania kutoa taarifa ambazo wana uhakika nazo ili kuepuka kusababisha taharuki na hofu kubwa. “Tunaomba wananchi wasisambaze taarifa ambazo hawana uhakika nazo au kufahamu undani wa ukweli wake, kwani ni kosa la jinai kisheria na siyo maadili ya uandishi wa habari kuisumbua jamii.”
Taarifa hiyo imemalizia kwa kutoa wito kwa wazazi na walezi kutimiza wajibuwao wa kuwatunza na kuwalinda watoto wao na kuwasihi Polisi nao kuchunguza matukio yanayotajwa, na kuwataka waongeze ulinzi katika maeneo mbalimbali nchini ili kuendelea kuaminika kwa wananchi na wajione wako salama.
0 Maoni