TANAPA yatakiwa kushirikiana na TTB kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi

 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayeshughulikia Utalii - Nkoba Mabula amelitaka Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) katika kutangaza vivutio vya Utalii ndani na nje ya nchi ili kuvutia watalii wengi zaidi kutembelea Tanzania.

Mabula ameyasema hayo Julai 16, 2024 alipotembelea Ofisi za Makao Makuu ya Shirika hilo yaliyopo mtaa wa Majengo jijini Arusha na kuwapongeza kwa jitihada nzuri wanazozifanya za kutangaza vivutio vya vya utalii vilivyomo katika hifadhi 21 zinazosimamiwa na taasisi hiyo mama ya Uhifadhi nchini.

Akiwa katika kikao na Menejimenti ya Shirika hilo Mabula alisema, “TANAPA mnafanya kazi nzuri sana ya kutangaza utalii, kwani nimewaona kwenye maonesho mengi ya ndani na nje ya nchi mkinadi vivutio vyetu, hivyo niwasisitize shirikianeni na TTB kutangaza zaidi ili adhma ya watalii milioni 5 iliyopo kwenye Ilani ya Chama Tawala iweze kutimia.”

Awali, akimkaribisha na kutoa wasilisho la mwenendo mzima wa utalii ndani ya TANAPA kwa Naibu Katibu Mkuu huyo, Kamishana Msaidizi wa Uhifadhi, Maendeleo ya Biashara - Jully Lyimo alisema, “Shughuli za utalii zinazofanyika katika Hifadhi za Taifa Tanzania zimeendelea kuzaa matunda huku tukishuhudia ongezeko la watalii kila mwaka. Ongezeko hili ni kutokana na juhudi kubwa tulizowekeza katika kutangaza utalii ndani na nje ya nchi.”

Aidha, Kamishna Lyimo aliongeza kuwa shirika lina mazao mbalimbali ya utalii na lina mpango wa kuendelea kuvumbua mazao mengine mapya ya utalii ili watalii wanapotembelea Hifadhi za Taifa wawe na muda mwingi wa kukaa hifadhini ili kuliongezea Taifa mapato.

Hata hivyo, TANAPA inaendelea kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuyafikia masoko ya kimkakati duniani ya Brazil, Urusi, na China.

Baada ya kikao na Menejimenti ya TANAPA, Bw. Mabula alipata wasaa wa kutembelea Hifadhi ya Taifa Arusha na kujionea vivutio kadhaa katika hifadhi hiyo kama vile maporomoko ya maji ya Tululusia, Kreta ya Ngurdoto, Mlima Meru na Ziwa Momella lilisheheni ndege aina ya Flamingo wakubwa kwa wadogo.

Na. Philipo Hassan- Arusha

Chapisha Maoni

0 Maoni