Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Selemani Jafo, amepongeza Wakala wa Vipimo (WMA) kwa utendaji kazi mahiri na wenye weledi na kutoa wito kwa Taasisi nyingine zilizo chini ya Wizara hiyo kuiga mfano wake.
Ametoa pongezi hizo mapema leo, Julai 17, 2024 jijini Dodoma
alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la Makao Makuu ya Wakala
huo, lililopo eneo la Medeli.
Mheshimiwa Jafo amekiri kuridhishwa kwa kiwango kikubwa na
utendaji kazi wa WMA kupitia ziara zake alizofanya kukagua kazi mbalimbali
zinazotekelezwa na Wakala huo, ambapo awali (Julai 11, 2024) alitembelea Kituo
cha Uhakiki wa Vipimo kilichopo Misugusugu Mkoa wa Pwani na kujionea utendaji
kazi wake.
“Kwa ujumla nimeridhishwa sana na utendaji wa Wakala huu na
niwatake wengine waige mfano huu mzuri. Wito wangu, waendelee kufanya kazi kwa
lengo la kuhakikisha Serikali ya Dkt. Samia Suluhu Hassan inapata mafanikio
makubwa katika maeneo yote,” amesema.
Ameongeza kusema kuwa, pongezi zake kwa Wataalamu wa Wakala
wa Vipimo pia ni kutokana na kuonesha mfano mwema sana kwa kutumia mapato ya
ndani, kujenga jengo hilo, hali
inayothibitisha kuwa Taasisi hiyo ni miongoni mwa zile zinazofanya vizuri.
Akieleza zaidi, Waziri Jafo amesema lengo la ziara yake
kukagua jengo hilo ilikuwa kujiridhisha kuhusu thamani ya fedha iliyowekezwa
katika ujenzi huo pamoja na kasi ya utekelezaji wake ambapo kwa ujumla amesema
ameridhishwa kwa kiasi kikubwa.
Akifafanua, amesema kuwa, kwa hatua iliyofikiwa katika
ujenzi, ambayo ni asilimia 81.5 anaamini jengo hilo linaweza kukamilika hata
kabla ya muda uliopangwa ambao ni Januari 2025.
Hata hivyo, pamoja na kumpongeza Mkandarasi anayetekeleza
ujenzi huo, Kampuni ya M/S Mohamed Builders chini ya Mshauri Elekezi, Chuo
Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Mbeya (MUST), amewataka kuhakikisha
wanakamilisha kazi hiyo kwa wakati na viwango stahiki kama inavyotarajiwa.
Katika hatua nyingine, Waziri Jafo amewasisitiza watendaji
wa WMA kuzingatia maelekezo aliyoyatoa kwao katika ziara yake ya awali, kuhusu
kukagua maeneo yote yanayohusu ukaguzi hususani mita za umeme na maji kabla
hazijafungwa kwa wateja ili kulinda haki za walaji ambao ni wananchi.
“Naelekeza mita zote za umeme na maji lazima zifikishwe
Wakala wa Vipimo ili kuzipima kuangalia uthibiti wake kwa lengo la kuwapunguzia
gharama wananchi. Isije mtu akafungiwa mita ambayo haina ubora, mwisho wa siku
akalipa bili isiyo stahiki,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA,
Joseph Maliti ametoa ahadi kwa Waziri kuwa Wakala utahakikisha maelekezo yake
yote yanatekelezwa.
Naye Mwakilishi wa Mkandarasi, Mhandisi Justin Kyando
amesema wana uhakika watakamilisha ujenzi kwa wakati kwani wako katika hatua za
ukamilishaji.
Mradi wa Ujenzi wa Jengo la Makao Makuu ya Wakala wa Vipimo
jijini Dodoma ulianza Julai 2, 2022 na unatarajiwa kukamilika Januari 2025
ambapo gharama yake ni shilingi bilioni 6.17.
Na Veronica Simba - WMA
0 Maoni