Hospitali ya Taifa Muhimbili-Mloganzila imekuwa hospitali ya
kwanza ya Umma nchini kuanzisha huduma mpya ya kutibu magonjwa ya ngozi kwa
kutumia teknolojia mpya na ya kisasa ya mwanga (Laser).
Kauli hiyo imetolewa na Naibu Mkurugenzi Mtendaji
MNH-Mloganzila, Dkt. Julieth Magandi alipokuwa kizungumza na waandishi wa
habari kuhusu kuanzishwa rasmi kwa huduma hiyo iliyoanza kutolewa rasmi
Muhimbili Mloganzila .
“Tunawashukuru wenzetu wa Korea Kusini kwa kutusaidia
kuwapatia mafunzo ya namna ya kutumia tiba mwanga kutibu magonjwa mbalimbali ya
ngozi, sasa wataalam wetu wana uwezo wa kutosha kutoa huduma hizi,” ameongeza
Dkt. Magandi.
Dkt. Magandi ameongeza kuwa hospitali ina wataalam
waliobobea katika magonjwa ya ngozi sambasamba na vifaa tiba vya kisasa ambavyo
vinapatikana MNH Mloganzila kitu ambacho kinafanya huduma hii kufanyika kwa
ufanisi.
Kwa upande wake Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Ngozi Dkt.
Andrew Foi amesema huduma hii inaweza kusaidia kutibu magonjwa ya ngozi
yaliyoshindikana kwenye matibabu ya kawaida na kuboresha muonekano wa ngozi.
Dkt. Foi amesema huduma ya tiba mwanga inahusisha kutibu magonjwa ya ngozi ikiwemo vitiligo, pumu ya ngozi, saratani ya ngozi, kuondoa tatoo, viotea, michirizi katika sehemu mbalimbali za mwili na nywele ikiwemo usoni (Phototherapy).
0 Maoni