Kikundi cha Maafisa na Askari wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi
wa Tanzania, Vyombo Vya Usalama na Taasisi za Kiraia za serikali ya Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania kimeshiriki katika ufunguzi rasmi wa Zoezi la 13 la Medani
la Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki "FTX Ushirikiano Imara
2024" linalofanyika katika Chuo cha Kijeshi cha Maafisa Gako Nchini Rwanda
tarehe 13 Juni 2024.
Mkuu wa Kamandi ya Jeshi la Nchi Kavu Meja Jenerali Fadhil Omary
Nondo ambaye amemuwakilisha Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali John Jacob
Mkunda amesema kuwa tangu kuanzishwa kwa
zoezi hilo kumekuwa na mafanikio makubwa kwa kuwa Vyombo Vya Ulinzi, Usalama na
Taasisi za Kiraia kutoka nchi wanachama wa EAC vimekuwa vikifanya mafunzo na
mazoezi ya pamoja katika nyanja mbalimbali ikiwemo Ulinzi wa Amani, kukabiliana
na Majanga ya kibinadamu,ugaidi na
uharamia wa kwenye maziwa na baharini ili kujiweka tayari kukabiliana na changamoto
mbalimbali pindi zitakapojitokeza.
Kikundi kutoka Tanzania kimeundwa na Jeshi la Ulinzi la
Wananchi wa Tanzania, Polisi, Uhamiaji, Zimamoto na Uokozi pamoja na Taasisi
mbalimbali za Kiraia chini ya uongozi wa
Brigedia Jenerali Said Hamis Said ambaye pia ndiye Kamanda wa Vikosi vya
Jumuiya ya Afrika Mashariki vinavyoshiriki zoezi hilo.
Zoezi Ushirikiano Imara 2024 limefunguliwa rasmi na Waziri wa Ulinzi wa Rwanda Mheshimiwa Juvenal Marizamunda.
0 Maoni