Mradi wa Bomba la Mafuta la EACOP waboresha maisha ya wanavijiji

 

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) umeweza kubadilisha maisha ya waguswa zaidi ya 9,000 pamoja na jamiii iliyokatika maeneo yaliyopitiwa na mradi huo, kiasi cha kuacha alama chanya ya maendeleo na uchumi ambayo haitosahaulika kwa jamii husika.

Akiongea na waandishi wa habari hivi karibuni katika warsha iliyofanyika kwenye Hoteli ya Sea Cliff Jijini Dar es Salaam kuelezea maendeleo ya mradi huo, Afisa Mawasiliano wa Mradi huo Abass Abraham amesema wameshalipa madai ya waguswa kwa zaidi ya asilimia 99.

“Tumesha lipa madai ya waguswa zaidi ya asilimia 99, na asilimia chache iliyobakia haijalipwa kwa sababu mbalimbali zikiwemo za kifamilia, kama vile za suala la mirathi baada ya mhusika kufariki kabla ya malipo kutolewa,” alisema Abass.

Amesema kwamba kwa waguswa ambao nyumba zao zimepitiwa na ujenzi wa bomba hilo, walipatiwa uamuzi wa kuchagua kulipwa fidia ama kujengewa nyumba ambapo jumla ya waguswa 339 wamejengewa nyumba.

“Waguswa 339 walioridhia kujengewa nyumba wamesha jengewa nyumba zao za kisasa zenye kutumia nishati ya umeme, tenki la kuhifadhia maji, choo cha kisasa pamoja na jiko la kisasa,” alisema Abass na kuongeza, “Kila mguswa alifidiwa nyumba kwa idadi ya vyumba kama aliyokuwa nayo, lakini safari hii ni ya kisasa iliyojengwa kwa teknolojia ya zege kutoka Afrika Kusini.”

Amesema kutokana na nyumba hizo kuwa za kisasa tofauti na nyumba zao za zamani ambazo zilijengwa kwa udongo na hazina umeme, waguswa hao kwanza walipatiwa elimu na kitabu cha muongozo wa matumizi sahihi ya nyumba hizo ili zidumu.

Amesema mbali na fidia za nyumba waguswa walihakikishiwa upatikanaji wa chakula salama kwa kuwagaiwa bure, na kuongeza kuwa pia mradi wa EACOP umetoa ajira kwa jamii inayouzunguka kwa kuzingatia suala la usawa wa kijinsia.

“Waguswa wa mradi huu pia wamepatiwa elimu ya kilimo ambayo imewasaidia kuweza kulima na kupata mavuno mengi na bora, hali ambayo imesaidia katika kuwabadilishia maisha yao kwa kupata kipato zaidi kutokana na kilimo,” alisema Abass.

Amesema mradi pia umesaidia kuvinyanyua vikundi vidogo vidogo vya biashara katika maeneo yaliyoguswa, umejenga na kukarabati madarasa ya shule, umegawa madawati, umejenga barabara kwa kiwango cha changarawe na kupanua miondombinu ya maji katika eneo la Tanga.

Kuhusu maandalizi ya awali, Abss amesema wameshafanya kwa kuchukua maeneo ya kujenga kambi na ujenzi umeshaanza, “kwa upande wa uwekaji mabomba wataalam wanasema kuwa ni jambo rahisi ambapo kwa sasa tayari uzalishaji wa mabomba umeshaanza.”

Kwa upande wake Bi. Fatuma Msumi ambaye ni Mkuu wa Idara ya Uhamasishaji Jamii EACOP, mradi umepitia katika mikoa nane, wilaya 25, Halmashauri 28, Kata 117 na vijiji 233 pamoja na zaidi ya vitongoji zaidi ya 450.

Amesema kwamba tangu mwaka huu uanze wameonana na wadau wa mradi huu wapatao zaidi ya 24,000 kupitia mikutano ya hadhara, katika majadiliano mbalimbali waliyofanya na kati ya hao watu waliokutana nao asilimia 44 ni wanawake.

“Tunapenda zaidi kuchukua takwimu za wanawake ni idadi gani kwasababu tunajua mila na desturi zetu wanawake mara nyingi hawaendi kwenye mikutano, kwa hiyo sasa tunapoangalia ni idadi gani ya wanawake tunaangalia taarifa hizi zimewafikia makundi gani,” alisema Bi. Fatuma.

Bi. Fatuma amesema lengo kuu la kuangalia ushirikishaji wa makundi yote ya jamii katika mradi huo ni kuhakikisha fursa zinapojitokeza makundi yote yanazipata kwa usawa na wala hawaachwi nyuma wanawake ama vijana.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unaurefu wa kilomita 1,443 kutokea Kabale, wilayani Hoima Uganda hadi Chongoleani Mkoani Tanga Tanzania, ambapo kwa upande wa Tanzania ndio mrefu zaidi una kilomita 1,147 na kwa Uganda ni kilomita 296.

Chapisha Maoni

0 Maoni