Baba wa watoto waliokufa kwa moto Arusha naye afariki

 

Idadi ya waliofariki katika ajali ya moto iliyoua watoto watatu wa familia moja jijini Arusha imeongezeka baada ya baba wa watoto hao askari CRI wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), Zuberi Hassan Msemo naye kupoteza maisha.

Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, Jeradi Nonkwe, amethibitisha kutokea kwa kifo hicho, na kusema marehemu huyo alikuwa ni baba wa watoto watatu waliofariki kwa ajali ya moto iliyotokea Juni 22, 2024.

Watoto waliofariki ni Mariam Zuberi (9), Salma Zuberi (7) na Bisma Zuberi (3) ambapo mama wa watoto hao, Jasmine Khatibu (33), Mariam Mussa (60), Mwanaid Aldina (50), Mussa Msemo (34), AbdulKarim Ramadhan (9) na dada wa kazi aliyefahamika kwa jina moja la Ester (20) wanaendelea na matibabu.

Kamanda amesema kuwa baba huyo amefariki jana Jumapili Juni 23, 2024 wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mount Meru jijini Arusha, na kueleza kuwa chanzo cha kifo chake ni kuvuta moshi mwingi alipokuwa akijaribu kuwaita watu waje wasaidie kuwaokoa.


Chapisha Maoni

0 Maoni