Malori ya mradi wa bomba la mafuta ghafi dereva akilewa gari haliwaki


Katika kuepusha ajali zinazoweza kusababishwa na uzembe wa madereva Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), umefunga mifumo maalum ya kuwadhibiti madereva wanaosafirisha mabomba ya mradi huo wasikiuke sheria za usalama barabarani.

Afisa Mawasiliano wa Mradi huo Abass Abraham, amesema kwamba malori yanayotumika kusafirisha mabomba hayo yamefungwa mfumo ambao, iwapo dereva atakuwa amelewa gari litagoma kuwaka na kumuepusha na uwezekano wa kusababisha ajali.

“Malori tunayoyatumia kusafirisha mabomba ya mradi wa EACOP, yamefungwa mfumo unaoweza kubaini kwamba dereva amelewa na endapo atajaribu kuwasha gari ili aendeshe akiwa mlevi gari litagoma kuwaka,” alisema Abass.

Kama hiyo haitoshi, amesema malori hayo pia yanamfumo ambao unaweza kubaini iwapo dereva amechoka ama anasinzia, na kutoa taarifa ambapo dereva husika atapigiwa simu na kuagizwa atafute sehemu aegeshe gari ili apumzike.

“Katika mradi huu tumezingatia usalama na ulinzi wa mazingira kwa hali ya juu, na hata hayo mabomba yanayotumika kwenye mradi huu nayo yatafungwa mifumo ya mawasiliano ili kuyalinda dhidi ya uharibifu,” alisema Abass.

Mabomba tunayotumia ambayo yamezungushiwa ganda la juu, yana mfumo unaoweza kutoa taarifa kwenye vituo vya usimamizi iwepo kuna mtu anafanya shughuli za kibinadamu karibu na bomba zinazoweza kuhatarisha, alisema Abass.

“Licha ya kuwa na mfumo huo wa ulinzi utakaozuia uharibifu, pia mabomba hayo yatakuwa na mfumo wa umeme utakaokuwa unazalisha joto ili kuhakikisha mafuta ghafi yanayosafirishwa ndani ya bomba hayagandi,” alisema Abbas.

Abass amesema bomba la kusafisha mafuta ghafi ambalo litafukiwa chini aridhini litatumia upana wa mita 30 tu, ambapo baada ya kufukiwa eneo litakalopita bomba hilo juu yake utarejeshwa uoto wa asili ili kulinda mazingira.

Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi la Afrika Mashariki (EACOP) unaurefu wa kilomita 1,443 kutokea Kabale, wilayani Hoima Uganda hadi Chongoleani Mkoani Tanga Tanzania, ambapo kwa upande wa Tanzania ndio mrefu zaidi una kilomita 1,147 na kwa Uganda ni kilomita 296.


Chapisha Maoni

0 Maoni