Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) imetaka watendaji
wakati wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura Mkoani Kigoma
kuhakikisha wanatunza vifaa vya uandikishaji ili vikaweze kutumika maeneo
mengine nchini.
Hayo yamesemwa na Mwenyekiti wa Tume Huru ya Taifa ya
Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Rufaa Jacobs Mwambegeke wakati akifungua mafunzo ya siku
mbili kwa Waratibu wa Uandikishaji wa mkoa, Maafisa Waandikishaji, Maafisa
Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Jimbo, Maafisa Uchaguzi, Maafisa Ugavi na
Maafisa TEHAMA wa halmashauri yaliyoanza leo tarehe 20 hadi 21 Juni,2024 Mkoani
Kigoma.
“Kwa kusisitiza, ni muhimu kutekeleza majukumu yenu kwa
umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji hasa
ikizingatiwa kuwa, vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa sana na
vinatarajiwa kutumika katika maeneo mengine ya uandikishaji nchini,” alisema
Jaji Mwambegele.
Amesema kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi
kutapelekea athari kubwa katika ukamilishaji wa zoezi hili muhimu na amewataka
kuzingatia maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ili muweze kuyafanyia kazi
wakati zoezi litakapokuwa limeanza.
Aidha, Jaji Mwambegele amesema matokeo bora ya zoezi hili
yanategemea uwepo wa ushirikiano mkubwa kati ya watendaji wote wa uboreshaji,
serikali, vyama vya siasa na wadau wengine wa uchaguzi.
“Ninawasihi muwe na ushirikiano mzuri na wa karibu na Tume
wakati wote mtakapokuwa mnatekeleza majukumu yenu na ikiwa mnahitaji ufafanuzi
au maelekezo yeyote, msisite kuwasiliana na Tume,” alimema Jaji Mwambegele.
Mapema kabla ya kuanza mafunzo hayo, washiriki walikua kiapo
cha kujitoa uanachama na kile cha kutunza siri mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Rose
Kangwa.
Mafunzo hayo yanahusisha namna ya ujazaji wa fomu pamoja na
kutumia mfumo wa kuandikisha wapiga kura (Voters Registration System - VRS) ili
waweze kupata uelewa wa pamoja utakaowapa fursa ya kutumia kwa ufasaha mfumo
huo pamoja na vifaa vingine vya kuandikisha wapiga kura.
“Mafunzo haya, yanawajengea umahiri wa kuwafundisha Maafisa
Waandikishaji Wasaidizi ngazi ya Kata kisha nao watatoa mafunzo hayo kwa
Waendeshaji wa Vifaa vya Bayometriki na Waandishi Wasaidizi ambao ndio
watahusika na uandikishaji wa wapiga kura vituoni,” alisema Jaji Mwambegele.
Aidha, Maafisa TEHAMA watapatiwa mafunzo maalum ya jinsi ya
kukabiliana na changamoto mbalimbali za kiufundi (Troubleshooting) endapo
zitajitokeza wakati wa zoezi la uandikishaji wa wapiga kura vituoni.
Katika hatua nyingine, Jaji Mwambegele amewaambia watendaji
hao kuwa wakati wa uboreshaji wa Daftari mawakala wa vyama vya siasa
wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikisha wapiga kura jambo ambalo
litasaidia kuleta uwazi katika zoezi zima lakini pia mawakala hao watasaidia
kutambua waombaji wa eneo husika hivyo kupunguza kutokea kwa vurugu zisizokuwa
za lazima.
Jaji Mwambegele alitoa angalizo kwa mawakala hao kutoka vyama vya siasa kuwa hawaruhusiwi kuwaingilia watendaji wakati wote wa utekelezaji wa majukumu yao vituoni.
Tume imetangaza uzinduzi wa zoezi la Uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Mpiga Kura utafanyika tarehe 01 Julai, 2024 mkoani Kigoma ambapo Mgeni rasmi anataraji kuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Majaliwa Kassim Majaliwa na kauli mbiu ya uboreshaji ni “Kujiandikisha Kuwa Mpiga Kura Ni Msingi Wa Uchaguzi Bora.”
0 Maoni