WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya wahakikishe kila halmashauri inaanzisha operesheni maalum za
ulinzi kwa watu wenye ualbino.
“Operesheni hizi zihusishe vikosi vya usalama ili
kuhakikisha ulinzi wa watu wenye ualbino dhidi ya mashambulizi na vitisho hii
ni kwa sababu katika kuzuia unyanyasaji na mauaji ya watu wenye ualbino,
Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa zinawajibika katika usimamizi, ulinzi na
utoaji wa huduma kwa watu wenye ualbino,” amesema.
Ametoa wito huo leo (Alhamisi, Juni 20, 2024) wakati akitoa
taarifa kuhusu kupinga ukatili dhidi ya watu wenye ualbino wakati wa kipindi
cha maswali ya Papo Kwa Papo kwa Waziri Mkuu, Bungeni, jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amezitaka Mamlaka za Mikoa na Wilaya zihamasishe
ushiriki wa jamii katika kuhakikisha ulinzi na haki za watu wenye ualbino kwani
vitendo vya mauaji ya albino vinahusisha mtandao wa watu na siyo mtu mmoja
mmoja tu.
Amesema Serikali tayari imeshajenga mifumo thabiti ya
udhibiti na suala lililobaki ni ushiriki wa makundi yote ya jamii katika
kuhakikisha vitendo hivyo viovu vinakomeshwa hapa nchini. “Kwa kutambua jukumu
tulilonalo kama Taifa, nitumie nafasi hii kuyataka makundi na taasisi
mbalimbali katika jamii kuendelea kushiriki kikamilifu katika mapambano dhidi
ya vitendo hivyo vya ukatili.”
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amewaomba viongozi wa
dini waendelee kukemea kukemea maovu yanayotendeka nchini hususan mauaji kwa
watu wenye ualbino kwani kuwepo kwa matukio hayo kunaonesha upotofu wa maadili
na kukosa hofu ya Mungu.
“Nitumie nafasi hii kuwaomba viongozi wetu wa dini tuungane
pamoja kupambana na mauaji ya watu wasiokuwa na hatia hata kidogo. Ninawasihi
watumie majukwaa yao ya ibada kuwahubiria waumini wao waachane na vitendo hivyo
vya ukatili ambavyo hata Mwenyezi Mungu anavikataza. Watu wenye ualbino wana
haki ya kuishi kama walivyo watu wengine,” amesisitiza.
Waziri Mkuu amesema waganga wa jadi nchini kote wanapaswa
kushiriki kikamilifu katika kampeni za kupinga mauaji ya watu wenye ualbino.
“Wakati umefika kwenu nyote kushirikiana na Serikali katika kutokomeza imani
potofu zinazochangia mauaji haya. Ninawasihi sana elezeni wazi kwamba hakuna
tiba wala mafanikio yanayoweza kupatikana kwa kutumia viungo vya watu wenye
ualbino.”
Pia amelitaka Baraza la Tiba Asili na Tiba Mbadala lifanye
usajili wa waganga wa jadi na vituo vyao sambamba na aina ya huduma wanayoitoa
kwa wateja wao ili kuweza kudhibiti huduma holela isiyofuata misingi ya utu na
haki za binadamu.
Mbali na hao, amewataka viongozi wa kimila kutoka kila kona
ya Tanzania washiriki kikamilifu katika kukemea na kupinga mauaji ya watu wenye
ualbino. “Ninawaomba viongozi wetu wa kimila wakiwemo machifu washirikiane na
Serikali kwa kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama pindi wanapopata fununu za
mipango au vitendo vya mauaji ya watu wenye ualbino katika maeneo wanayoishi.”
Ili kuhakikisha matukio ya aina hiyo hayatokei, Waziri Mkuu
amelielekeza Jeshi la Polisi lichukue hatua za haraka pindi linapopata fununu
ya uwepo wa njama za utekaji na mauaji ya watu wenye ualbino.
Pia ametaka liendelee kufanya operesheni ya kuwakamata wote
waliotajwa na watakaotajwa kuhusika kwenye matukio ya aina hii ili kuua mtandao
mzima wa wahalifu. “Polisi jamii ishirikishwe kikamilifu ili kupata taarifa
zote muhimu katika maeneo husika na watoa taarifa wote walindwe ipasavyo,”
amesisitiza.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema lengo la Serikali ni
kuwalinda wananchi walioathirika kwa kuwa wanahitaji kuwekwa mahali salama kwa
kuwa bado wanakuwa wana hofu kutokana na madhila yaliyowafika.
“Sera yetu ya Serikali ni kuwalinda wote wenye ulemavu wa
aina yoyote ili washiriki shughuli za maendeleo huku tukihakikisha wanakuwa
salama. Malengo yetu ni kutoa uhakika wa maisha yao wakati wote.
“Bado tunaendelea kutafuta njia mbadala ikiwemo kuwachanganya
ili wasijione wametengwa. Tumeanza kuwachanganya katika shule za msingi na
sekondari ili nao washiriki pamoja kwenye shughulimbaliza kijamii na michezo
bila kujali ulemavu wao.”
Alikuwa akijibu swali la Rashid Shangazi (Mbunge wa Mlalo) ambaye alimtaka Waziri Mkuu aeleze ni kwa nini Serikali inapanga kuwaweka waathirika kwenye kambi ilhali ni kinyume na haki ya kuwa huru kama ilivyoelezwa kwenye ibara ya 15(1) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni