Takribani vijana 192 kunufaika na ajira za ulinzi wa misitu

 

Hayo yamesemwa na Msaidizi wa Mhifadhi Mkuu wa Shamba la Miti Saohill Said Singano akizungumza katika zoezi la usahili wa vijana watakaochaguliwa kujiunga na kikosi cha kupambana na kuzuia majanga ya moto pindi yanapotokea katika maeneo ya misitu ikiwa ni msimu wa kiangazi, usahili ulioanza kufanyika katika makao makuu ya shamba tarehe 18 Juni 2024.

Amesema kuwa kila mwaka shamba limekuwa na utaratibu wa kuajiri wafanyakazi kwa mkataba wa miezi sita kuanzia Julai mpaka Disemba huku lengo kuu ikiwa ni kuhakikisha misitu na maeneo yanayolizunguka shamba yanakuwa salama dhidi ya majanga ya moto huku akisisitiza vijana wanaopata nafasi ni wale wanaokidhi sifa zilizowekwa.

Aidha, amewataka vijana wanaopata nafasi kufanya kazi kwa bidii na uadilifu na kufuata maelekezo wanayopewa na viongozi wao muda wote wanaokuwa kazini na kusisitiza kwa wale waliokosa nafasi kuendelea kushirikiana na shamba katika shuguli za ulinzi wa msitu kwani kuna kazi nyingi zinazoendelea ndani ya shamba.

Sambamba na hilo ametoa wito kwa wananchi wanaolizunguka shamba  kuendelea kuhakikisha wanafuata taratibu zilizowekwa za uanzishwaji wa moto ili kuepusha moto usiotarajiwa ikiwepo kuandaa mashamba kwa wakati na kuacha kurina asali kwa kutumia moto na kuwataka kutumia njia za kisasa wanazoelekezwa na shamba.

Kwa upande wake Mkuu wa kitengo cha ulinzi wa msitu katika Shamba la Miti Saohill Mhifadhi Murya Sawa amesema kuwa zoezi la kukabiliana na majanga ya moto katika misitu ni jukumu la kila mwanachi hivyo linahitaji uzalendo na ukakamavu ili kukabiliana na hatari inayoweza kujitokeza na kuwataka wananchi wote kuendelea kuchukua tahadhari dhidi ya moto hatarishi.

Naye Kaimu Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Wilaya ya Mufindi Sajenti Ashery Kitundu amesema kuwa Jeshi la Zimamoto limekuwa likishirikiana na Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania kupitia Shamba la miti Saohill ili kuhakikisha kuwa elimu dhidi ya majanga ya moto hususani wa misituni inawafikia wananchi wengi Wilayani Mufindi ili kuhakikisha wanakuwa na tahadhiri dhidi ya moto hatarishi wa msituni.

Zoezi la usaili linatarajiwa kuendelea katika vituo vyote vya tarafa zote za Shamba Tarafa ya Kwanza Irundi, Tarafa ya Tatu Ihalimba pamoja na Tarafa ya Nne Mgololo.



Chapisha Maoni

0 Maoni