NEEC kuwajengea uwezo wanawake na vijana wajasiriamali

 

Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC), limesema litaendelea kuwajengea uwezo wanawake na vijana wanaoanzisha biashara pamoja na kuziendeleza biashara zilizokwisha anzishwa na kundi hilo.

Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es Salaam na Katibu Mtendaji wa NEEC Bi. Beng’i Issa wakati akihitimisha mafunzo ya Kuongeza kasi ya Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabia nchi na Kuhuisha Biashara za Kilimo Ndogo na za Kati kwa Wanawake na Vijana.

Mafunzo hayo yaliyofadhiliwa na Benki ya Kiarabu ya Uchumi na Maendeleo kwa Afrika (BADEA) na kuendeshwa na Taasisi ya Umoja wa Mataifa ya Mafunzo na Utafiti (UNITAR) yalianza Novemba 2023 na kuhitimishwa rasmi leo kwa washiriki kupewa vyeti.

Bi. Beng’i amesema NEEC ambayo pia imeshirikiana na UNITAR kwenye mafunzo hayo, itaweka rekodi ya washiriki wote 50 walionufaika na mafunzo hayo yaliyohusu kuwajengea uwezo wa kuomba mitaji kwenye taasisi za kifedha, ili kuhakikisha inaendelea kuwasaidia kutimiza ndoto zao.

Amesema katika kuhakikisha ujasiriamali unapewa kipaumbele NEEC imefanya mazungumzo Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia ili kuhakikisha somo la ujasiriamali linaanza kusomeshwa kuanzia ngazi ya msingi hadi ya juu ili kuwajengea uwezo wahitimu.

Kwa upande wake Ofisa wa Mradi wa UNITAR, Bw. Michael Adalla, amewataka wahitimu wa mafunzo hayo kutumia vizuri elimu waliyopatiwa katika kufanikisha kuanzisha na kuendeleza biashara zao na kuwa mabalozi wazuri kwa kutoa elimu hiyo kwa wengine.

Pia aliiishukuru Benki ya Kiarabu ya Uchumi na Maendeleo kwa Afrika (BADEA) kwa kuwezesha mafunzo hayo na NEEC kwa kushirikiana kwa karibu na UNITAR katika kuendesha mafunzo hayo, pamoja na benki ya CRDB kwa kuhudhuria katika hatua ya kuomba mitaji ili kutoa mwanga kwa wahitimu.

Ofisa wa Mradi wa UNITAR, Bw. Michael Adalla, akiongea na Katibu Mtendaji wa NEEC Bi. Beng’i Issa wakati wakuhitimisha mafunzo ya Kuongeza kasi ya Uhimilivu wa Mabadiliko ya Tabia nchi na Kuhuisha Biashara za Kilimo Ndogo na za Kati kwa Wanawake na Vijana leo Jijini Dar es Salaam.

Chapisha Maoni

0 Maoni