Teknolojia mbadala kuimarisha mtandao wa barabara ikiwemo
ujenzi wa madaraja imara na madhubuti itaendelea kutumiwa nchini na Wakala ya
Barabara za Vijijini na Vijijini - TARURA.
Yameelezwa hayo na Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais -
TAMISEMI Mhandisi Rogatus Mativila mbele ya waandishi wa habari katika banda la
maonesho ya TARURA kwenye mkutano wa 30 wa wahandisi Afrika.
“TARURA wanaonesha utaalamu wanafanya ikiwemo ujenzi wa
‘structure’ mbalimbali za kupitishia maji, wanajenga kwa mawe teknolojia ambayo
inapunguza gharama,” amesema.
Akizungumza namna Serikali ilivyojipanga kurejesha
miundombinu iliyoharibiwa na mvua zilizoanza kunyesha tangu Oktoba, 2023 na
zinazoendelea hadi sasa, Naibu Katibu Mkuu Mativila amebainisha kwamba bado
kuna sehemu nyingi mvua zinaendelea
kunyesha, miundombinu mingi imeharibika, mvua zilizokuja hazikuwa za kawaida
kama miaka mingine.
Hata hivyo amesema wameshafanya tathimini na zinahitaji
kiasi cha Tsh. Bil. 2 kurejeresha
miundombinu iliyoharibiwa na mvua na Serikali ipo tayari kutoa fedha hizo
Naye, Msimamizi wa Teknolojia Mbadala TARURA – Makao Makuu
Mhandisi Mshauri Pharels Ngeleja amesema tayari wamejenga madaraja 256 kwa
teknolojia ya mawe yaliyogharimu Tsh. Bil. 13.
“Teknolojia ya mawe tunatumia pia kujenga barabara, kuna Km.
26.18 zimekamilika Mkoani Mwanza, Kigoma na Rukwa, pia kwenye barabara zetu
zingine tunatumia teknolojia za Ecoroad, Ecozyme na Polymer”.
“Tumejenga barabara ya Sawala Km. 13 Mkoani Iringa, Chamwino
- Dodoma pia tunaendelea na hizi teknolojia, Dodoma kuna barabara inaitwa
daraja dogo tumekamilisha.Miradi hii ipo maeneo mbalimbali ambapo tunaendelea,”
amesema Mhandisi Ngereja.
Vilevile amesema TARURA kupitia kitengo cha mambo ya
mazingira wanaendelea pia kufuatilia kwa ukaribu athari za mabadiliko ya tabia
nchi ili kujiimarisha zaidi katika ujenzi wa miundombinu yake.
TARURA imeweza kujenga barabara kwa kutumia teknolojia ya Ecoroad, Ecozyme na Polymer katika barabara ya Chamwino Km. 7,Itilima Km. 5, Sawala-Mkonge Km. 10 na Daraja dogo -Dodoma Km.1.
0 Maoni