Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ametoa wito kwa jamii ya Watanzania kuacha kuwanyanyapaa watoto na watu wanaoishi na Usonji, magonjwa ya mfumo wa fahamu pamoja na matatizo ya akili.
Pia amewataka wazazi na walezi wenye watoto wenye changamoto
za ukuaji au uelewa watafute ushauri kwa wataalam wa afya ili watoto wao waweze
kufaidika na huduma zilizopo katika umri
mdogo.
"Wataalam wetu muendelee kuongeza juhudi katika
kuelimisha jamii kuhusu magonjwa haya ili watu wengi zaidi waweze kunufaika na
huduma."
Ametoa wito huo leo ( Jumapili 28, Aprili 2024) alipokuwa
akizungumza baada ya kushiriki mbio fupi
za hisani za Run 4 Autism Tanzania, zilizofanyika katika viwanja vya The Green
Ground Oysterbay Jijini Dar es Salaam.
Kadhalika ameiagiza Wizara ya Afya kuongeza vituo vya huduma
za uchunguzi hasa utambuzi wa mapema wa ugonjwa wa usonji na matatizo mengine
ambayo yanaweza kubainika wakati watoto wanapoenda kwenye kliniki kila mwezi.
"Wizara ya Afya na Ofisi ya Rais TAMISEMI zihakikishe
uwepo wa huduma jumuishi zinazoweza kuleta tija kwa kina mama na watoto ambao
wanazaliwa na magonjwa ambayo yanaweza kubainika mapema."
Aidha, ameitaka Wizara ya Elimu iendelee kongeza kasi ya
upanuzi wa utoaji wa huduma za Elimu Jumuishi pamoja na kuongeza wigo wa
mafunzo na vyumba vya madarasa katika shule nyingine ili watoto wenye ulemavu
wasitembee umbali mrefu kwenda shule.
Pia amevitaka vyombo vya habari, wasanii na wanajamii kwa
ujumla kutumia kila fursa kuielimisha
jamii kuhusu masuala mbalimbali ya afya.
"Wanahabari tumieni kalamu zenu kuelimisha jamii kuhusu
afya na udhibiti wa magonjwa mbalimbali yakiwemo magonjwa ya akili."
Naye, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu amesema Wizara ya Afya
kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Muhimbili (MUHAS), imeanzisha Shahada ya
kwanza ya Sayansi ya Mazoezi tiba ya kusaidia mawasiliano (Speech pathology),
Tiba Kazi (Occupational therapy) na Tiba Viungo (Physiotherapy) na shahada ya
kwanza ya Sayansi ya Saikolojia ya Kitabibu (Clinical Psychology) kuanza mwaka
huu 2024.
"Lengo la kuanzishwa kwa shahada hizi ni kuhakikisha
kuwa, huduma za utengemao zinapewa kipaumbele cha juu na Serikali."
Awali, Mwanzilishi na Mkurugenzi Mtendaji wa Lukiza Autism
Foundation ambao ndio waandaaji wa mbio hizo amesema lengo la mbio hizo ni
kuchangisha fedha kiasi cha Shilingi Milioni 50 kwa ajili ya kutekeleza mkakati
wa miaka mitano kuanzia 2024 hadi 2028 wenye lengo la kukuza Ustawi wa Kila
Mtoto mwenye viashiria vya usonji.
"Mkakati huu ni kwa ajili ya kuongezea nguvu mipango ya Serikali kupitia Wizara ya Elimu na Afya kwa kuboresha uwezo wa walimu wa shule za Chekechea katika kubaini viashiria vya usonji kwa watoto."
Ugonjwa wa Usonji kwa kiingereza Autism, ni ugonjwa ambao
kwa mujibu wa shirika la afya duniani, WHO
hukumba mtoto mmoja kati ya kila watoto 160 duniani.
Usonji ni tatizo la kibaiolojia analopata mtoto anapokuwa tumboni mwa mama yake na dalili huonekana kuanzia umri wa miaka mitatu na kuendelea.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni