Somo la uhifadhi laeleweka wengine 422 wahama leo Ngorongoro

 


Serikali imefafanua kuwa itaendelea  kuzingatia utoaji wa haki zote kwa wananchi wanaoamua kwa hiari kuhama kutoka kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kupisha uhifadhi na kwenda kwenye maeneo  wanayoyataka  ikiwa ni pamoja na maeneo yaliyotengwa.

Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ngorongoro  Murtalla Mbillu ametoa kauli hiyo alfajiri ya leo Aprili 7, 2024  Makao Makuu ya  zamani ya Hifadhi ya Ngorongoro wakati alipokuwa akiwaaga jumla ya wananchi 422  kwenye walioamua  kuondoka kwa hiari kwenye Hifadhi ya Ngorongoro kupisha uhifadhi na kwenda kwenye maeneo waliyoyachagua.

“Bila shaka mnatambua  kuwa pamoja na Serikali kuwalipa fidia  na motisha bado mkifika  katika Kijiji cha Msomera mtapata huduma zote za msingi ikiwa ni pamoja na kupatiwa nyumba kwenye kiwanja cha ukubwa wa ekari 2.5 na ekari tano za kufanya  shughuli za kilimo, eneo la malisho pamoja na huduma za elimu,afya, umeme na maji,” amesisitiza Mbillu.

Amefafanua kuwa zoezi  la kuhama  ni zoezi la hiari ambapo mtu mwenyewe  bila kushinikizwa  na mtu ana hiari ya kuondoka lakini asitokee mtu wa kuwarubuni na kuwadanganya  watu walioamua  kuhama  kwa  hiari yao kwa kuwa kwa kufanya hivyo watakuwa wanafanya jinai na hatua za kisheria  zitachukuliwa dhidi yake.

Mwakilishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii  na Msemaji wa  Wizara hiyo, John Mapepele amewapongeza wananchi walioamua kwa hiari  kuondoka kupisha uhifadhi  huku akimshukuru rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Mhe, Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa maono yake makubwa na dhamira ya kuboresha maisha ya wananchi.

Aidha, amesema dhamira ya Serikali ni kutaka wananchi wake wanapata haki zao za msingi za kuishi maisha bora na kupata huduma zote za kijamii kama elimu na  afya bila  kubughudhiwa na mtu.

Kaimu Kamishina wa Hifadhi ya Ngorongoro Victoria Shayo amewataka wananchi hao walioamua kuhama kwa hiari kuwa mabalozi wazuri kuwashawishi wananchi walibaki kuchukua maamuzi sahihi ya kupisha uhifadhi.

Akitoa taarifa ya zoezi hilo Kaimu Meneja wa  Mradi kuhamisha wananchi wa Hifadhi ya Ngorongoro, Flora Assey kaya 60 zenye watu 353 zimeelekea Kijiji cha Msomera wakati kaya 13 zenye watu  69 zimeelekea Meatu Simiyu  na kaya zilizobaki  zimeelekea simanjiro  na Arusha.




Chapisha Maoni

0 Maoni