Mbunge wa Rufiji na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais - Tawala
Mikoa na Serikali za Mitaa Mhe. Mohamed Mchengerwa ameshiriki utoaji wa misaada
ya chakula na malazi kwa waathirika wa mafuriko yaliyotokea katika Wilaya ya
Rufiji.
Mhe. Mchengerwa
akiwa na Uongozi wa CCM Mkoa wa Pwani
pamoja na Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dkt. Mehmet Gulluoglu wametoa
misaada hiyo kwa wakazi wa Mohoro walioathirika na mafuriko ambao
wamejihifadhiwa katika Shule ya msingi Mohoro.
Akizungumza na wananchi Mchengerwa amesema "Tunatambua
athari zilizoletwa na mafuriko haya kaya nyingi zimeathirika nilikwishatoa
Sh.Milioni 40 kwa ajili ya ununuzi wa mbegu kwa wananchi walioathiriwa mashamba
yao na mvua lakini kama hiyo haitoshi rafiki zangu wameniunga mkono na sasa
tumeleta vyakula pamoja na magodoro kwa kaya zinazoishi katika shule hii."
Ameongeza kuwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan anafahamu
taarifa hizo na ametuma Timu ya Maafa kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kufika eneo
hilo na kukuendelea kutoa misaada ya kibinadamu katika kata 12 za Wilaya ya
Rufiji na kufanya tathmini ya kina ya athari ya mafuriko hayo.
Naye, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Pwani Mwinshehe Mlao ametoa
rai kwa Mkuu wa Wilaya ya Rufiji kuhakikisha anasimamia vyema misaada hiyo kwa kuweka
mpango wa kuhakikisha wale wenye uhitaji zaidi ndio wanaopata na sio wale wenye
kuhitaji nyongeza.
Kwa upande wake, Balozi wa Uturuki nchini Tanzania Dkt.
Mehmet Gulluoglu amesema wameguswa na adha hiyo iliyowapata wananchi wa Rufiji
na ametoa msaada wa vyakula na bahasha ya pole kwa familia zilizothirika zaidi.
CHANZO: Ofisi ya Rais- TAMISEMI
0 Maoni