Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) amewapongeza wadau wa utalii nchini kwa kuwa sehemu ya mafanikio ya sekta hiyo katika kipindi hiki ambapo utalii umekuwa na mchango mkubwa katika kuchangia kwenye mapato ya fedha za kigeni.
Mhe. Kairuki ametoa kauli hiyo jana mjini Arusha akiwa na
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Hassan Abbasi kwenye mkutano
wa pamoja baina ya Wizara na wadau wa sekta ya utalii ambao ni Chama cha
Waongoza Utalii, Wakala wa Usafirishaji Utalii, Vyama vya Wamiliki wa Huduma za
Malazi na Vyama vya Wabeba Mizigo kujadili masuala mbalimbali ili kuboresha
sekta hiyo.
Aidha, amesema wadau wa utalii wana mchango mkubwa katika
uchumi wa taifa ambapo amefafanua kuwa sekta hiyo inachangia takribani asilimia
zaidi ya 25 ya mapato ya fedha za kigeni na kutoa fursa za ajira na kuchochea
ukuaji wa sekta nyingine muhimu.
Katika mkutano huo Waziri Kairuki amemtaka Mtendaji Mkuu wa
Bodi ya Utalii (TTB) ambaye ameteuliwa hivi karibuni bwana Ephraim Mafuru
kushirikiana na wadau mbalimbali wa utalii nchini ili kuendelea kuvitangaza
vivutio vya utalii duniani.
Ametoa wito kwa waongoza watalii kuwa wazalendo kwa kuwa wao
ndiyo mabalozi wa taifa huku akisisitiza kuwa wageni hukaa nao kwa muda mwingi
hivyo ni muhimu kutoa taarifa sahihi.
Akiongea katika kikao hicho, Muongoza utalii, Hope Tumaini
ambaye amekuwa kwa zaidi ya miaka 15 ameishukuru Serikali kwa kazi kubwa
inayoifanya huku akiomba Serikali kutoa mafunzo maalum kwa waongoza watalii
hususan wanawake.
Mhe. Waziri amesema kuanzia mwakani Serikali itatoa mafunzo
ya utalii kuanzia kwenye ngazi ya Sekondari ambapo wadau wa utalii pia
watahusishwa katika maandalizi ya mitaala ya utalii ili mafunzo hayo yawe na
tija.
Katika mkutano huo baadhi ya mambo ambayo yamejadiliwa na kupatiwa ufumbuzi wakati mengine
yakiendelea kufanyiwa kazi.
Baadhi ya mambo ambayo yamepatiwa ufumbuzi leo ni pamoja
na kupunguza ada ya leseni ya waongoza Utalii iliyokuwa USD 50 kila
mwaka ambapo sasa itakuwa laki moja kila baada ya miaka 3 ada hiyo itaanza
Januari 2025 pia malipo ya ada ya leseni hiyo ya waongoza watalii ya dola za
kimarekani 50 sasa itaanza kulipwa kwa shilingi za kitanzania kuanzia Julai mwaka huu.
Aidha, Mhe. Kairuki amefuta viingilio kwa waongoza watalii
katika mageti ya hifadhi kwa waliolipia
leseni zao za usajili.
Wadau hao wa Sekta ya
Utalii wametumia mkutano huo na Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii
kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa
kuleta mabadiliko chanya katika kipindi kifupi cha uongozi wake, huku wakisifu
kasi ya sasa ya utendaji wa Wizara.
Awali akimkaribisha Waziri Kairuki katika mkutano huo Dkt.
Abbasi amesisitiza kuwa katika kipindi
hiki Serikali itakuwa karibu na wadau kwenye kila hatua ili kuhakikisha sekta
inasonga mbele kwa maslahi ya wadau na taifa kwa ujumla.
Na. John Mapepele- Arusha
0 Maoni