Serikali ya Awamu ya Sita imedhamiria kuboresha na kuimarisha
mazingira ya biashara nchini ili kuendana na azma ya kufanya mageuzi ya
kiuchumi na viwanda kwa ajili ya kuleta maendeleo endelevu ya jamii.
Hayo yamebainishwa jana na Waziri wa Viwanda na Biashara,
Dkt. Ashatu Kijaji akifungua kikao cha Wizara yake na Wakuu wa Idara ya
Viwanda, Biashara na Uwekezaji wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali
za Mitaa kilichofanyika mkoani Morogoro.
Dkt. Kijaji amesema kuwa Serikali ya Awamu ya Sita
inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa
Tanzania jitihada zake ni kutengeneza mahusiano mazuri na Wafanyabiashara ili
kukuza uchimi wa taifa.
“Dunia imeshaingia katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda ambayo yanajikita
katika matumizi makubwa ya teknolojia na uharaka wa utoaji wa huduma, watu
kukutana kidigitali na uwepo wa maarifa ya kutosha na yasiyo na mipaka kwa
jamii ili kuongeza uzalishaji wa bidhaa na huduma kwa njia za kidigitali,”
amesisitiza Dkt. Kijaji.
Aidha, Dkt. Ashatu Kijaji amewataka Wizara na Maafisa
Biashara wa Mikoa na Wakuu wa Idara za Biashara, Viwanda na Uwekezaji kukaa
pamoja na kujadili mustakabali wa kukumbushana wajibu wa kutekeleza Sera,
Sheria, Kanuni pamoja na taratibu zinazohusu biashara na viwanda katika
Halmashauri zao.
“Nimewaiteni ninyi nikitambua kwamba ndiyo mlioaminiwa
kuongoza sehemu na Idara za Viwanda Biashara na Uwekezaji katika Mamlaka zenu
ili tuyatafsiri na kuyaelewa kwa pamoja majukumu mliyonayo, matarajio na matokeo
tarajiwa ya uanzishwaji wa Sehemu na Idara hizo katika maeneo yenu,” amesema
Dkt. Kijaji.
Naye Katibu Mkuu Ofisi ya Raisi Tawala za Mikoa na Serikali
za Mitaa -TAMISEMI Ndg. Adolph Ndunguru amesema kuwa mpango wa maendeleo wa
serikali ni kuifikisha nchi katika uchumi shindani na kuboresha masoko ya
bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Kuhakikisha
tunachokizalisha kinauzwa, lakini pia kuongeza tija katika uwekezaji ili mpango
wetu wa kutengeneza uchumi shindani ufanikiwe kwa kiwango kikubwa,” amesema
Ndg. Ndunguru.
Awali akitoa neno la
utangulizi, Afisa Mtendaji Mkuu wa BRELA, Bw. Godfrey Nyaisa amewapongeza Wakuu
wa Idara za Viwanda, Biashara na Uwekezaji kutoka Mamlaka za Mikoa na Serikali
za Mitaa kwa kushiriki Mkutano.
“Kikao kazi hiki kina
lengo la kuwajengea uelewa Wakuu wa Sehemu na Idara za Viwanda, Biashara na
Uwekezaji kutoka katika Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kuhusu Sheria,
Kanuni na Taratibu za sajili na utoaji wa leseni zinazosimamiwa na BRELA na
namna ambavyo tunaweza shirikiana katika kutekeleza majukumu ya kukuza sekta ya
biashara na uwekezaji nchini,” amesema
Bw. Nyaisa.
Kikao kazi hiki kimehudhuriwa na Wakuu wa Sehemu na Idara za
Viwanda Biashara na Uwekezaji katika Sekretarieti za mikoa na Mamlaka za
Serikali za mtaa wapatao 200, wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara ya
Viwanda na Biashara na Wakurugenzi kutoka Ofisi ya Rais TAMISEMI na
kinatarajiwa kuhitimishwa tarehe 7 Aprili, 2024 mkoani Morogoro.
0 Maoni