Mkurugenzi Mtendaji wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
Prof.Mohamed Janabi amekutana na Afisa Mkuu kutoka Shirika lisilo la Kiserikali
la Marekani ReSurge International kwa lengo la kuendeleza ushirikiano na
kujengeana uwezo katika kufanya upasuaji rekebishi kwa watu wenye changamoto
mbalimbali ikiwemo waliopata ajali ya kuungua moto na wenye misuli iliyokakamaa
kutokana na majeraha.
Akizungumza wakati wa kikao hicho Prof. Janabi amesema
Muhimbili ina nguzo tatu muhimu ambazo ni Huduma, Elimu na Utafiti hivyo kama
Hospitali ya Taifa haina budi kutekeleza kwa vitendo kwakuwa ni wajibu wetu.
Ameeleza kuwa MNH itaendelea kuboresha ushirikiano na wadau
mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi ili kuendelea kuwajengea uwezo wataalam
wake zaidi katika kutoa huduma za kibingwa na ubingwa bobezi hapa nchini.
“Ili kuendena na mabadiliko ya sayansi na teknolojia katika
tiba, naamini katika kujifunza na kuongeza elimu kwa kubadilishana uzoefu
kutoka kwa watua ambao wanajua zaidi,” amesema Prof. Janabi.
Kwa upande wake, Daktari Bingwa wa Upasuaji wa MNH, Dkt.
Ibrahim Mkoma, amesema mwanzoni mwa mwaka huu MNH ilishirikiana na wataalam
kutoka shirika hilo na kufanya kambi maalum ya siku tano iliyohusisha upasuaji
wa urembo na upasuaji wa matibabu (Cosmetic and Reconstructive Surgery) kwa
wagonjwa nane.
0 Maoni