Kampuni kubwa zinazojishughulisha na masuala ya utalii
duniani zimevutiwa kuwekeza nchini Tanzania katika huduma za malazi,
usafirishaji na utangazaji utalii.
Hayo yamesemwa leo na Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe.
Angellah Kairuki (Mb) katika Maonesho ya Utalii ya ITB yanayoendelea jijini
Berlin Ujerumani.
“Nimefurahi kukutana na kampuni kubwa ya TUI (TUI Group)
yenye Makao Makuu nchini Ujerumani ambayo ina hoteli zaidi ya 400 duniani, meli
za kitalii 16, mashirika ya ndege matano na zaidi Mashirika 1,200 ya usafiri,”
Mhe. Kairuki amesisitiza.
Amefafanua kuwa
kampuni hiyo imewekeza Zanzibar na hadi kufikia mwezi Juni mwaka huu itazindua
hoteli yao ya tisa lakini kwa upande wa Tanzania Bara inaendelea kufungua
safari za ndege ili kuleta watalii katika hifadhi zilizopo nchini Tanzania.
Waziri Kairuki
ametumia fursa hiyo kuihamasisha kampuni hiyo ili iongeze uwekezaji kwa upande
wa Zanzibar na Tanzania Bara katika huduma za hoteli, ndege za kukodi kwa lengo
la kuhakikisha Tanzania ina ndege nyingi zaidi za kwenda maeneo mbalimbali ya
vivutio vya utalii.
“Tumewaomba waendelee kushirikiana na sisi kama Serikali
katika kutangaza utalii wa Tanzania katika ndege zao,hoteli zao na tuweze
kufanya kampeni mbalimbali za kutangaza utalii kwa pamoja,” Waziri Kairuki
amesema.
Aidha, Mhe. Kairuki amekutana na kampuni inayosafirisha
watalii zaidi ya milioni 1.2 duniani yenye Makao Makuu Marekani
na Puertoriko ambayo imeonyesha utayari na kuanzia mwezi Mei mwaka 2024
italeta Wakala wa Usafirishaji zaidi ya 40 kutembelea maeneo mbalimbali nchini
Tanzania.
Waziri Kairuki pia amekutana na kufanya mazungumzo na Kampuni
ya Kimataifa ya Utangazaji ya Expedia Group pamoja na kampuni kutoka Slovakia
ambayo inapeleka watalii duniani kwa zaidi ya asilimia 85 kutoka nchini humo na
ina matangazo katika luninga zao na kujadili namna ya kushirikiana katika
kuandaa matangazo ya vivutio vya utalii.
Vilevile Mhe. Kairuki amekutana na Wadau wa usafirishaji
watalii wenye ulemavu kutoka nchini Afrika Kusini kuona namna bora ya
kutengeneza vifurushi (package) vya kutalii kwa ajili ya watu wenye ulemavu
kutembelea nchini Tanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Utalii
Tanzania (TTB), Damas Mfugale amesema ushiriki wa Tanzania kwenye Maonesho hayo
ni chachu ya kuongeza idadi ya watalii nchini.
Naye, Mmoja wa Washiriki kutoka nchini Tanzania ambaye ni
Mkurugenzi wa Kampuni ya African Qeen Adventures, Alice Manupa amemshukuru Rais
Samia kwa kuwa Royal Tour imeweza kuitangaza Tanzania kimataifa.
Na. Mwandishi Wetu-Berlin
0 Maoni