Taasisi ya Utafiti wa
Wanyamapori Tanzania (TAWIRI)
imebainisha kuwa, wadudu hususani nyuki ni wanyamapori wenye mchango mkubwa
katika uhifadhi wakiwa na jukumu kubwa
la uchavushaji mimea ambayo hutumiwa kama chakula na wanyamapori wakubwa na
wadogo.
Akitoa elimu ya wadudu kwa wanafunzi walio tembelea banda la
TAWIRI wakati wa maonesho ya siku ya wanyamapori Duniani, yaliyofanyika Mjini
Babati tarehe 3 Machi 2024, Mtafiti Kezia Oola alisema, mbali na jukumu la
uchavushaji, wadudu wana mchango mkubwa katika uhifadhi mfumo Ikolojia.
Kezia alibainisha kuwa mdudu (Dung beetle) anasaidia
utawanyaji na uoteshaji mbegu mwituni, umeng'enyaji virutubisho vya udongo hasa
vinyesi vya wanyama, (decomposition) na uongezaji mbolea kwenye udongo (soil
fertilization). Kwa kufanya hivi husaidia kuwezesha makazi ya wanyama wengine.
Pia, alieleza kuwa uwepo wa wadudu katika uhifadhi inasaida
mzunguko wa chakula (food chain) ambapo kuna wanyama wadogo na ndege
wanaotegemea wadudu kwa asilimia kubwa kama chakula chao akiwemo mnyama Mhanga
(Aardvark) na wanyama hawa huliwa na wanyama wengine.
Kwa upande wake Mtafiti Kipemba Ntiniwa amebainisha kuwa
katika uhifadhi nyuki anachukua nafasi kubwa katika uchavushaji tofauti na
wadudu wengine kwa kuwa Nyuki wanakaa kwa makundi makubwa ambapo mzinga mmoja
unakuwa na nyuki zaidi ya elfu ishirini.
"Nyuki ni mchavushaji mkuu wa kuendeleza uwepo wa mimea
mbalimbali katika uhifadhi," alieleza Kipemba.
Ameongeza kuwa, nyuki wanatumika kupunguza migongano
baina ya Binadamu na Wanyamapori
hususani tembo (Mitigation of Human-Wildlife Conflicts) ambapo uzio wa mizinga ya nyuki unaweza
kuwazuia tembo kuingia maeneo/mashamba ya wananchi na kufanya uharibifu.
Vilevile, Kipemba amebainisha faida nyingine za nyuki
kiuchumi na kijamii ni pamoja na kuongeza kipato kupitia utalii wa nyuki (Apitourism), uuzaji mazao ya nyuki
ambayo ni asali, nta, chavua, sumu ya nyuki na maziwa ya nyuki pamoja na
kusaidia uwepo na usalama wa chakula kupitia uchavushaji.
Ikumbukwe, katika Maonesho
hayo yalifanyika kwa siku tano kuanzia tarehe 28 February hadi tarehe Mosi Machi ,2024 Watafiti wa
TAWIRI mbali na kutoa elimu katika banda
la maonesho, waliitembelea Shule ya Sekondari
Babati Day na Kutoa elimu juu ya
umuhimu wa wadudu, tafiti za
wanyamapori na uhifadhi endelevu
katika kukuza utalii nchini.
0 Maoni