Mkuu wa Wilaya ya Kilwa Mhe. Christopher Emil Ngubiagal
amesema Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA ni taasisi
iliyoleta mapinduzi makubwa katika Sekta ya Utalii na kuwa chanzo kikubwa cha
mapato ya Serikali na wazawa wa wilaya hiyo kutokana na maboresho ya
miundombinu ya utalii katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa
kisiwani na Songo Mnara yanayopelekea watalii wengi kutembelea Hifadhi hiyo.
Komredi Ngubiagal ameyasema hayo akizungumza na waandishi wa
habari wilayani humo ikiwa ni siku moja baada ya meli iliyobeba watalii 146
kutia nanga katika Hifadhi ya Urithi wa Dunia ya Magofu ya Kilwa kisiwani na
Songo Mnara.
"Naipongeza Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
chini ya Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa awamu ya sita kwa kuona sasa utalii
katika wilaya ya Kilwa ni vyema tupeleke taasisi inayoitwa TAWA ili kusudi
ikasimamie, ikaendeleze, ikaboreshe hii Sekta nzima ya utalii ya wilaya ya
Kilwa," amesema Mhe. Christopher Ngubiagal.
"Kwakweli kwasasa hivi unavyoona maendeleo makubwa
katika Sekta hii ya utalii Kilwa yameletwa na Taasisi ya TAWA, Leo ukifika
Kilwa kisiwani utaona mabadiliko makubwa katika miundombinu" ameongeza
Mkuu huyo wa wilaya.
Mhe. Christopher amesema awali kabla ya ujio wa TAWA wakazi
wa wilaya yake pamoja na watalii walikuwa wakipata adha ya kufika Kilwa
kisiwani kutokana na uduni wa miundombinu lakini baada ya kuingia TAWA
walipeleka boti za Kisasa ambazo zinawafanya watalii na wazawa hao kufika
hifadhini kwa raha mstarehe.
Aidha amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuongeza soko la utalii aliposhiriki filamu
ya Tanzania The Royal Tour ambayo imeleta mabadiliko makubwa ambayo hayajawahi
kutokea.
Naye Said Amri Said mkazi wa Kilwa kisiwani amekiri kuwa
ujio wa TAWA katika Hifadhi hiyo umechangia kuongeza idadi ya watalii ambapo
kupitia wageni hao wakazi wa eneo hilo wananufaika kiuchumi kwa kufanya
biashara ndogo ndogo ambazo zinawaingizia kipato.
Kwa upande wake Afisa Habari wa TAWA Beatus Maganja ametoa wito kwa wakazi wa wilaya ya hiyo kutumia fursa ya ujio wa Meli za watalii kujiongezea kipato kwa kuuza bidhaa pendwa kwa wageni kama vile vitu mbalimbali vya asili na kiutamaduni.
Na. Beatus Maganja- Kilwa
0 Maoni