WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali iko katika
hatua za mwisho za kukamilisha utaratibu wa malipo ya wananchi waliohamishwa
katika eneo la Nyantwali ili kupisha hifadhi na mapito ya wanyama.
“Naomba muwe watulivu, tathmini ilikwishafanyika na sasa
Serikali inakamilisha taratibu za mwisho za uhakiki ili kufanya malipo kwa
wananchi wote."
Mheshimiwa Majaliwa ameyasema hayo jana jioni (Jumatatu,
Februari 26, 2024) alipokuwa akijibu swali lililoulizwa na Mbunge wa Jimbo la
Bunda Mjini, Robert Maboto kuhusu malipo ya fidia kwa wakazi wa Nyatwali katika
mkutano wa hadhara uliofanyika katika viwanja vya shule ya msingi Miembeni.
Waziri Mkuu amesema kumekuwa na changamoto katika baadhi ya
maeneo ambayo wananchi wamekuwa wakitakiwa kulipwa fidia kwani baadhi yao
wamekuwa si waaminifu kwa kuleta taarifa zisizo sahihi na wengine kuweka
pingamizi juu ya utaratibu wa malipo.
Mapema, Waziri Mkuu alizindua mradi wa maji wa Misisi –
Zanzibar ulioko kata ya Sazira ambao umegharimu sh. milioni 733 na hadi kufikia
Januari, 2024 unahudumia wakazi 152,708 wa mjini Bunda.
Akitoa taarifa ya mradi huo, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka
ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Bunda (BUWSSA), Bi. Esther Gilyoma alisema
mradi huo umetokana na kukamilika kwa ujenzi wa mradi wa chujio la kutibu na
kusafisha maji Nyabehu ikiwa ni sehemu ya upanuzi wa mtandao wa huduma hiyo
kuweza kuwafikia wananchi wengi zaidi.
Alisema kazi ya ujenzi ilihusisha tanki la maji lenye ujazo wa lita 100,000 na maji hayo yanahudumia mitaa ya Nyasura ‘B’, Zanzibar na Misisi mjini Bunda.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni