Mageuzi makubwa yaliyofanyika kwenye sekta ya Afya nchini
kupitia Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan
yameivutia Serikali ya Jimbo la Kilifi kutoka Kenya ambao wamefika kujifunza
namna Tanzania ilivyofikia hatua hiyo.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Afya Jimbo hilo Mhe. Peter
Samwel Mwarogo akiwa na Wabunge wa Kamati ya Afya ya Jimbo hilo ambao
wametembelea Hospitali ya Taifa Muhimbili kuona mageuzi kupitia huduma,
uwekezaji vifaa tiba, uboreshaji miundombinu na utawala.
"Tumekua tukisikia maboresho ya huduma Tanzania
hususani Hospitali ya Taifa Muhimbili hivyo tumekuja kujifunza mambo mengi
mtambuka ili tukaboreshe sekta ya Afya kwa ujumla wake katika Jimbo letu,"
amesisitiza Mhe. Mwarogo.
Ameongeza kuwa ni muhimu kujifunza kutoka Tanzania kupitia "Muundo
wa Kusini Kusini" ambapo mazingira yao na Tanzania yanafanana hivyo
kurahisisha utekelezaji wa yote waliyojifunza.
Kwa upande wake Mwenyekiti Kamati ya Bunge ya Afya wa Jimbo
hilo Mhe. Edward Zero, amesema wameona mambo mengi ambayo ni chachu kwao kwenda
kuyafanyia kazi.
Pamoja na hayo wamejadiliana na Menejimenti ya Hospitali
kuhusu usimamizi wa Hospitali, kusomesha watalaam, ununuzi wa dawa na vifaa
tiba, malipo ya huduma kwa makundi mbalimbali.
Aidha, wameelezwa kuhusu uendeshaji wa mtambo wa kuchoma taka, uendeshaji Kliniki za wagonjwa wa kulipia, uwajibikaji wa watumishi, uendeshaji Idara ya dharura, radiolojia na masuala mengine mengi.
0 Maoni