Rais Mstaafu Mzee Ali Hassan Mwinyi afariki dunia

 

Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ametangaza kutokea kifo cha Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili Mzee Ali Hassan Mwinyi, aliyefariki dunia leo Februari 29, 2024 majira ya saa 11 jioni katika Hospitali ya Mzena Jijini Dar es Salaam alipokuwa akipatiwa matibabu ya ugonjwa wa Saratani ya mapafu.

Rais Dkt. Samia amesema kwamba Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi amekuwa akipatiwa matibabu tangu Novemba mwaka jana huko London nchini Uingereza, na baadae kurejea nchini na kuendelea na matibabu katika hospitali ya Mzena hadi leo umauti ulipomfika.

Rais Dkt. Samia ametoa pole kwa familia, ndugu jamaa na marafiki na watanzania wote kwa msiba huu mkubwa, na kutangaza siku saba za maombolezo ambapo kuanzia kesho bendera zote zitapepea nusu mlingoti.

Rais Samia ameeleza kwamba Hayati Mzee Ali Hassan Mwinyi atazikwa tarehe 2, Machi, huko Unguja visiwani Zanzibar na kuongeza kuwa taratibu za mazishi zitatangazwa baadae.

Chapisha Maoni

0 Maoni