Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto
Biteko amesema kuwa kazi ya uchorongaji wa visima vya Jotoardhi nchini Tanzania
itaanza mwezi Aprili mwaka huu ili kuweza kuhakiki rasilimali ya Jotoardhi
iliyopo kabla ya kuanza kwa shughuli za uzalishaji umeme kutokana na nishati
hiyo.
Dkt. Biteko amesema baada ya kutembelea vyanzo na mitambo ya
kuzalisha umeme wa Jotoardhi katika Mji wa Naivasha, Kaunti ya Nakuru nchini
Kenya.
“Tumekuja kwenye mitambo ya kuzalisha umeme unaotokana na
Jotoardhi inayomilikiwa na kampuni ya uzalishaji umeme ya Kenya (KenGen) na
tumejionea jinsi walivyopiga hatua kwenye uendelezaji wa rasilimali hii kwani
tayari wanazalisha umeme wa Jotoardhi wa kiasi cha megawati zaidi ya 799,” amesema
Dkt. Biteko.
Amesema Tanzania kwa upande wake, tayari imeshatenga fedha
kwa ajili ya kuendeleza vyanzo vya Jotoardhi na kwamba kampuni ya KenGen mwezi
Aprili mwaka huu itakuwa mkoani Mbeya kwa ajili ya kuanza uchorongaji vyanzo
vya Jotoardhi katika eneo la Ngozi na Kiejo-Mbaka kwa kushirikiana na kampuni
ya Uendelezaji wa Jotoardhi Tanzania (TGDC).
Dkt. Biteko ameipongeza kampuni ya KenGen ya Kenya kwa hatua
kubwa waliyofikia katika uendelezaji wa Jotoardhi ambapo zaidi ya asilimia 60
ya umeme nchini humo unatokana na nishati hiyo.
Ametanabaisha kuwa, Tanzania imeamua kuongeza vyanzo vya
uzalishaji umeme na sasa nguvu kubwa inawekwa kwenye kuendeleza miradi kama
hiyo ya Jotoardhi ili kupata umeme wa kutosha kwa ajii ya wananchi.
Kwa upande wake, Meneja Mkuu wa Maendeleo ya Jotoardhi
katika kampuni ya KenGen, Peketsa Mangi amesema kuwa, nchi hiyo imekuwa na
ushirikiano mzuri na Tanzania katika kuhakikisha nchi hizo zinafanikiwa katika
uendelezaji wa Jotoardhi.
Ameishukuru Serikali ya Tanzania kwa kuipatia nafasi KenGen
kufanya kazi kwa pamoja na wataalan kutoka TGDC ili kuchimba visima vya uhakiki
wa rasilimali hiyo nchini na kueleza kuwa, kampuni hiyo ipo tayari kufanya kazi
husika kwa mafanikio.
Viongozi walioambatana na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa
Nishati kwenye ziara hiyo ni Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa
Afrika Mashariki, Mhe. Stephen Byabato, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati,
Mhandisi Felchesmi Mramba, Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Mhe. Benard Kibesse
na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Mhandisi Gissima
Nyamo-Hanga.
0 Maoni