Waziri Mkuu aweka jiwe la msingi soko la kisasa Tarime Mjini

  

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua na kuweka jiwe la msingi kwenye mradi wa ujenzi wa soko la kimkakati la Tarime mjini unaotarajiwa kugharimu sh. bilioni 9.6 hadi kukamilika kwake.

Akipokea taarifa ya ujenzi wa soko hilo jana jioni (Jumatano, Februari 28, 2024) Waziri Mkuu alielezwa kwamba mradi huo kwa sasa upo katika hatua ya umaliziaji na umefikia asilimia 82 ya utekelezaji.

Akitoa taarifa ya mradi huo mbele ya Waziri Mkuu, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji Tarime, Bi. Gimbana Ntavyo alisema shughuli zinazoendelea kwa sasa ni skimming, upakaji wa rangi, ufungaji wa milango kwenye maduka na vyoo na ufungaji wa mifumo ya umeme na maji kwenye jengo kuu la soko.

Alisema kazi nyingine ni uwekaji wa vigae na terazo kwenye vizimba, maduka ya nje na ndani na kwa upande wa kazi za nje, wanaendelea na uzalishaji wa paving na kuandaa maeneo ya kuzipanga.

“Hadi sasa malipo yaliyofanyika kwa mkandarasi ni sh. bilioni 5.77 na kwa mshauri ni sh. milioni 120.36 sawa na asilimia 60.86 ya gharama za mradi,” alisema na kuongeza: “Mradi huu utakuwa na maduka 325, vizimba 160, mabucha matatu, migahawa miwili, supermarket moja na Benki mbili.”

Akielezea manufaa ya mradi huo, Mkurugenzi huyo alisema mradi huo umetoa ajira za muda kwa watu 441 na utakapokamilika, Halmashauri inatarajia kuongeza mapato yake ya ndani kwa sh. milioni 588 kwa mwaka kutokana na mapato yatakayokusanywa.

Chapisha Maoni

0 Maoni