Zaidi ya sh bilioni 13 zatengwa kuendeleza Magereza- Majaliwa

 

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema katika mwaka wa fedha wa 2022/2023 na 2023/2024 Serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan imetenga shilingi bilioni 11.15 kwa ajili ya ununuzi wa magari 65 na kuendeleza ujenzi wa majengo ya magereza kwenye mikoa ya Morogoro, Kigoma, Arusha, Tabora, Dodoma na Pwani.

Ameyasema hayo jana, wakati akifunga Mafunzo ya Juu na Daraja la Pili kwa Askari wa Jeshi la Magereza, katika Chuo cha Mafunzo cha Magereza Ukonga (TCTA), ambapo ametumia fursa hiyo kuwataka wahitimu hivyo basi wote wakazingatie mafunzo waliyoyapata ili yakawe chachu katika kuboresha utendaji kazi wa majukumu yao ya kila siku.

Waziri Mkuu amesema Serikali imelipatia Jeshi la Magereza magari kwa ajili ya shughuli za utawala na usafirishaji wa mahabusu, hadi kufikia tarehe 22 Mei, 2023 tayari Serikali ilikuwa imeshalipa jumla ya shilingi bilioni 4.459 kwa ajili ya ununuzi wa magari 23, kati ya hayo, magari 18 ni ya utawala na matano ya mahabusu.

Mheshimiwa Majaliwa amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha Jeshi la Magereza limetengewa shilingi bilioni 6.691 kwa ajili ya ununuzi wa magari mengine 42 yatakayotumika kwa shughuli za utawala na utekelezaji wa jukumu la usafirishaji wa mahabusu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2023/2024 Serikali imetenga shilingi bilioni 2.769 kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa Magereza ya Gairo na Kilosa Mkoani Morogoro, Kakonko mkoani Kigoma, Kaliua na Igunga Mkoani Tabora, Karatu Mkoani Arusha, Msalato na Isanga Mkoani Dodoma, na Gereza la Kwa Mturuki lililopo Bagamoyo katika Mkoa wa Pwani.

Amesema miradi hiyo inatekelezwa sambamba na kuanza ujenzi wa magereza mapya ya Kiabakari Mkoani Mara, Mpimbwe katika Mkoa wa Katavi, Sengerema Mkoani Mwanza, Kyerwa Mkoani Kagera, Kingurungundwa Mkoani Lindi na Gereza la Mlolo lililoko Mkoani Iringa.

Pia, Waziri Mkuu amesema Serikali imetenga shilingi milioni 800 kwa ajili ya kuanza ujenzi wa Ofisi za Magereza katika Mikoa ya Geita, Kigoma, Lindi, Songwe na Tanga pamoja na shilingi milioni 225 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa nyumba za maafisa na askari wa Kikosi Maalum cha Kutuliza Ghasia Magerezani zilizopo Msalato Mkoani Dodoma.

“Licha ya hayo, Serikali imetenga shilingi milioni 285 kwa ajili ya kuboresha upatikanaji wa maji safi na salama katika magereza matano. Magereza hayo ni Ilagala lililoko Mkoani Kigoma, Mbarali Mkoani Mbeya, Kiteto katika Mkoa wa Manyara, Kingurungundwa Mkoani Lindi na Gereza la Kongwa Mkoani Dodoma.” Amesema kukamilika kwa miradi hiyo ya ujenzi kutahakikisha uwepo wa huduma bora, mazingira bora ya kazi, makazi bora na mahali salama pa kuhifadhi wafungwa na mahabusu.

Waziri Mkuu amesema sambamba na kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu na ununuzi wa vitendea kazi, Serikali imeendelea kutekeleza mikakati mahsusi ya kuendeleza rasilimali watu, katika mwaka 2021/2022 imetoa ajira 1,241 kwa Jeshi la Magereza.  “Katika mwaka 2022/2023 imetoa nafasi 734 hawa ni wale waliopo mafunzoni. Aidha, katika wa fedha 2023/2024 itatoa vibali vya ajira za watumishi 500 ili kupunguza changamoto ya upungufu wa watumishi.”

Vilevile, Waziri Mkuu amesema ili kuzidi kuongeza ufanisi katika Jeshi la Magereza jumla ya askari 8,337 na maafisa 3,540 wamepandishwa vyeo. Leo tunashuhudia Maafisa 607 wamehitimu kupitia mpango ya mafunzo uliotekelezwa kwa lengo la kuwajengea uwezo pamoja na kuwapandisha vyeo.

Amesema Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2020/2025 katika ibara ya 105 (n) inaielekeza Serikali kuliwezesha Jeshi la Magereza na Vyuo vya Mafunzo kuendelea na majukumu ya kutunza, kuhifadhi na kufundisha wahalifu na kuzalisha mali ili yaweze kujitegemea. “Serikali yetu imeendelea kuzingatia maelekezo hayo kwa vitendo.”

Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwahakikishia kwamba Serikali ya awamu ya sita itaendelea kutenga fedha kwa ajili ya kuimarisha utendaji wa Jeshi la Magereza kama ilivyoelekezwa. “Ilani ya Chama cha Mapinduzi inatekelezeka, imegusa sekta zote na sisi jukumu letu kama Serikali ni kuhakikisha kila kipengele kinafanyiwa kazi kwa ukamilifu.”

Kwa Upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani Hamad Masauni amesema Serikali imeendelea kutoa nafasi za ajira kwa vyombo vya Ulinzi na usalama ili kuendelea kuboresha mahitaji ya rasilimali watu pamoja na vitendea kazi.

Awali, Mkuu wa Jeshi la Magereza Kamishna Jenereali, Mzee Ramadhani Nyamka amesema jeshi hilo limeendelea kujiimarisha kwa kutoa mafunzo ya uongozi weledi na utimamu ili kuwa na jeshi imara pamoja na kuwezesha vitengo mbalimbali vya uzalishaji mali.

Akizungumza kuhusu mafunzo hayo Mkuu wa Chuo cha Mafunzo cha Magereza Ukonga, Willbard Kahumuza amesema Jumla ya Wanafunzi 607 wamefanikiwa kumaliza mafunzo hayo huku 86 wa ngazi ya juu na ngazi ya chini ni 521 na mmoja wa ngazi za juu akishindwa kuhitimu kwa sababu za kinidhamu.

CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu

Chapisha Maoni

0 Maoni