Mchengerwa ‘kuwafyeka’ wafanyakazi wazembe TAMISEMI

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe. Mohamed Mchengerwa amesema mtumishi wa umma kwenye Mamlaka za Serikali za Mitaa atakayefanya kazi kwa bidii na uadilifu atamlinda lakini yule mzembe katika kazi hatasita kumuondoa kwenye nafasi yake.

Mhe. Mchengerwa ameyasema hayo jana alipokuwa akizungumza na watumishi wa Sekretarieti ya Mkoa wa Shinyanga wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani humo. 

"Kuna watu wanafanya kazi kwa moyo wao wote na wanatimiza majukumu yao ipasavyo kwa weledi wa hali ya juu hawa nitawalinda na kuwakumbatia na kuhakikisha wanapata stahiki zao zote wanazostahili kwa wakati lakini wale wazembe na wabadhirifu nitawatoa kwenye nafasi zao mara moja,"amesema Mhe. Mchengerwa.

Amewahimiza kufanya kazi kwa weledi na kuisaidia serikali ili kuendelea kubaki kwenye nafasi yake.

"Katika utendaji wetu mshikamano baina ya chama na serikali ni muhimu sana hivyo lazima tufanye kazi za serikali vizuri ili chama kiendelee kuwa madarakani, kwa sababu chama kikiendelea kubaki madarakani na wewe ndio unaendelea kushika nafasi yako," amesema Mhe. Mchengerwa.

Wakati huo huo, Mhe. Mchengerwa amekabidhi magari manne kwa Halmashauri za mkoa huo kwa ajili ya usimamizi na ufuatiliaji wa shughuli za sekta ya afya.

Chapisha Maoni

0 Maoni