WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewapongeza viongozi na
wafanyakazi wa kampuni ya Azam Media Limited kwa mafanikio lukuki waliyopata
katika kipindi cha miaka 10 tangu kuanzishwa kwake.
Amesema kupitia urushaji wa matangazo yake, kampuni hiyo
imeweza kuwa mzalishaji mkubwa wa ajira kwa mawakala, wanataaluma mbalimbali,
imeinua wanamichezo katika soka, masumbwi, mbio za magari na pikipiki,
waigizaji wa filamu na wasanii wa muziki.
“Pia mmedhamini baadhi ya vilabu nchini, kuweka taa kwenye
baadhi viwanja vya michezo hali ambayo imewezesha mechi za soka kuchezwa usiku.
Msione hili kuwa ni jambo dogo, AZAM mko
mbali sana. AZAM mko juu,” alisema.
Alitoa pongezi hizo jana usiku (Jumapili, Desemba 17, 2023)
wakati akifunga maadhimisho ya miaka 10 ya Kampuni ya Azam Media Limited
yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam.
“Ninawapongeza Azam Media Limited kwa kuunga mkono jitihada
za Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutoa ajira kwa Watanzania
kuanzia mawakala hadi watangazaji. Tunakutambua Azam Media Limited kama mdau
mkubwa wa kutoa ajira,” alisema.
“Ninawapongeza pia kwa kubeba dhima ya kutunza mazingira
kupitia kampeni yenu ya ‘Mito ni Maisha Yetu.’ Ninawapongeza kwa kuona maeneo
nyeti na kuyaingiza kwenye mpango wenu wa mwaka yakiwa ni sehemu ya maadhimisho
ya miaka 10 ya Azam Media Limited,” alisema.
Alisema kupitia kampeni hiyo, walihamasisha makundi ya jamii
ili yashiriki kwenye uhifadhi na utunzaji wa vyanzo vya maji. “Lengo lilikuwa
ni kujenga uelewa ili jamii ifanye shughuli zao za kibinadamu kwa kuzingatia
umuhimu wa kutunza mito ambayo ni tegemeo kubwa kwa viwanda, kilimo, uzalishaji
wa umeme na matumizi ya nyumbani. Naungana nanyi katika hili kwani haya ndiyo
mambo ambayo Watanzania wanatakiwa kuyasikia na kuyazingatia wakati wote.”
Mapema, Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya
Habari, Nape Nnauye aliwapongeza wafayakazi wa kampuni hiyo kwa kuzingatia
weledi katika utendaji kazi wao.
“Azam Media ni miongoni mwa vyombo ambavyo vinanipa usingizi
mzuri kutokana na umahiri wao wa kazi, lakini pia niwapongeze kwa uwekezaji
mkubwa ambao umefanywa na kampuni hii ili kuhakikisha matangazo yao yanafika
maeneo mengi.”
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa AZAM Media Limited (AML), Tido
Mhando alisema maadhimisho hayo yalianza Januari mosi 2023 na waliyapanga
yafanyike kwa mwaka mzima ili waweze kuufahamisha umma nini kimefanyika ndani
ya miaka hiyo 10.
Alisema katika kipindi hicho, wameweza kujijenga kwa kiwango
kikubwa na kwamba hivi sasa wanasikika kote Afrika Mashariki na Kati.
Awali, Mkurugenzi Mkuu wa makampuni yanayounda Bakhresa
Group, Abubakar Bakhresa aliwashukuru Watanzania wote kwa jinsi walivyoipokea
kampuni ya AZAM na bidhaa zake.
“Tunaishukuru Serikali kwa kuweka milango yake wazi wakati
wote. Pia tunawashukuru wadau wetu tunaofanya nao kazi kama Bodi ya Filamu,
BASATA na wengineo,” alisema.
Alisema miaka 10 ya mwanzo ilikuwa ya kujifunza, ninaamini miaka 10 ijayo, itakuwa ya kuboresha na kuongeza mchango zaidi kukuza michezo na sekta nyingine.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni