Kampeni ya kuhamasisha wanafunzi wa vyuo vikuu kutembelea
Hifadhi ya Mpanga Kipengere iliyopo Mikoa ya Njombe na Mbeya ijulikanayo kwa
jina la "Mpanga/Kipengere Uni Retreat" imeanza kuonesha matokeo
makubwa kwa wanavyuo mbalimbali kuanza kutembelea Hifadhi hiyo.
Kampeni hiyo iliyozinduliwa Desemba 6, 2023 na Mamlaka ya
Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania - TAWA kupitia Pori la Akiba Mpanga/Kipengere
kwa kushirikiana na Chikanda Safaris & Adventure ilikuwa na lengo mahsusi
la kuwahamasisha wanafunzi wa vyuo vikuu nchini hususan vya Kanda ya Nyanda za
Juu kusini kutembelea Hifadhi hiyo ili kujionea vivutio mbalimbali vya kitalii,
maajabu yaliyopo na kujifunza mengi kuhusu historia adhimu iliyo ndani ya
Hifadhi hiyo
Katika kuonesha mwitikio,
Desemba 17, 2023 Hifadhi ya Mpanga Kipengere ilipokea kundi la kwanza la
wanafunzi wapatao 31 kutoka vyuo mbalimbali waliotembelea hifadhi hiyo
Akizungumza wakati wa mapokezi ya wanafunzi hao ndani ya
hifadhi hiyo, Kamanda wa Hifadhi ya Mpanga/Kipengere Donasian Makoi alisema
hifadhi ya Mpanga/Kipengere ina utajiri wa kipekee wa idadi kubwa ya maporomoko
ya maji yenye muonekano adhimu lakini pia pango la Chifu Mkwawa na eneo la uoto
wa asili lenye maua ya kipekee lijulikanalo kwa jina la ibaga mambo ambayo
yangeweza kuwa kivutio kikubwa katika safari yao ya Utalii.
TAWA kwa kushirikiana na Chikanda Safaris inaendelea kuwahamasisha watanzania wote kutembelea Hifadhi ya Mpanga/Kipengere hasa katika kipindi hiki cha msimu wa Sikukuu za Christmas na Mwaka Mpya.
Na. Beatus Maganja
0 Maoni