Mkurugenzu Mkuu wa Makumbusho ya Taifa la Tanzania, Dkt.
Noel Lwoga pamoja na wataalamu wake wamekutana na Mkurugenzi Mkuu wa Hospital
ya Taifa ya Muhimbili, Prof. Mohamed Janabi kwa lengo la kujadili namna bora ya
kuhifadhi Historia ya Sekta ya Afya na Hospital ya Taifa Muhimbili sambamba na
maendeleo ya Sekta ya Afya nchini.
Viongozi hao
wamekutana leo katika hospitali hiyo kwa lengo la kuangalia namna bora
ya kushirikiana katika utekelezaji wa jambo hilo kabla ya ujenzi wa majengo
mapya kuanza ambapo maandalizi ya utunzaji wa historia ya hospitali hiyo tangu
enzi za Sewahaji hadi sasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa MNH Prof. Mohamed Janabi amemueleza
Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Noel Lwoga kuwa, upembuzi yakinifu
kuhusu mradi huo unaratajia kuanza mapema mwaka 2024 ambapo katika ujenzi huo,
utunzaji historia ni kipaumbele namba moja, baadhi ya majengo yatabaki na
mojawapo litakuwa makumbusho ili kulinda historia yake kwa vizazi vijavyo
kuhusu hatua moja hadi nyingine ambazo Taifa limepitia katika maboresho ya
utoaji huduma katika sekta ya afya nchini.
“Hospitali ina majengo mengi ya zamani, yanayohitaji
ukarabati mkubwa na kutokukidhi mahitaji ya sasa ya utoaji huduma hivyo
tunahitaji kuijenga upya, katika hilo tutazingatia mambo mengi ikiwemo kuweka
huduma karibu ili kupunguza usumbufu kwa wagonjwa kutembea mita 500 kufuata
kipimo flani au huduma nyingine sehemu flani” amesisitiza Prof. Janabi.
Amesema, ujenzi huu utazingatia matumizi sahihi ya ardhi
ambapo eneo kubwa litakuwa wazi baada ya ujenzi huo kwani majengo yatakuwa
machache ukilinganisha na hali ilivyo sasa, kutakuwa na ramani moja
(comprehensive plan), kukidhi vigezo vingi vya kimataita vya utoaji huduma,
kuboresha na kuongeza huduma za kibobezi, kuwa kituo cha mafunzo ya huduma za
ubobezi na kuifanya Hospitali kuwa kituo cha Utalii Tiba (Medical Tourism Hub).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa Makumbusho ya Taifa, Dkt. Lwoga ameipongeza Menejimenti ya hospitali kwa kutambua umuhimu wa kuhifadhi historia ya taifa kwa ajili ya vizazi vijavyo na kuahidi kutoa ushirikiano wa hali ya juu kutimiza azma hiyo.
0 Maoni