Watu waliokufa maporomoko ya Hanang waongezeka na kufikia 69

 

Idadi ya watu waliokufa kwenye maporomoko ya matope ya Mlima Hanang yaliyotokea Wilayani Hanang mkoani Manyara yaliosababishwa na mvua, imeongezeka kutoka watu 65 hadi watu 69 kufikia leo Desemba 6, 2023.

Taarifa ya Serikali ya maendeleo ya hali baada ya maafa, iliyotolewa na Msemaji Mkuu wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi, imesema vifo vinne zaidi ni vya maiti zilizoopolewa kwenye tope za wanaume (2) na wanawake (2). Jumla maiti 68 zimeshatambuliwa na moja (1).

Amesema kwamba majeruhi waliobakia hospitalini hadi sasa ni 45 kutoka 117, ambapo katika hospitali ya Mkoa wa Manyara wapo 16, hospitali ya Wilaya (Tumaini) 18 na Kituo cha Afya Gendabi 11. Ni majeruhi mmoja tu ndiye alipoteza maisha akiwa hospitalini hadi sasa.

CHANZO CHA MAPOROMOKO

Haya yalikuwa ni maporomoko ya tope lililozoa mawe, magogo na kusukumwa na maji ya mvua iliyonyesha usiku huo. Haya si mafuriko ya maji kama ilivyozoeleka katika maafa mengine yanayosababishwa na mvua hapa nchini.

Kwa mujibu wa wataalamu wa Wizara ya Madini pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania, yaani Geological Survey of Tanzania (GST), hakukuwa na tetemeko la ardhi wala mlipuko wa volkano katika mlima Hanang.

Taarifa hiyo imeiongeza chanzo cha maafa haya ni kumeguka kwa sehemu ya mlima Hanang yenye miamba dhoofu iliyonyoya maji ya mvua na kuporomoka (landslide) na hivyo kutengeneza tope (mudflow).

Imeelezwa sehemu hiyo iliyonyonya maji ilizua mgandamizo na sehemu ya mlima ikashindwa kuhimili mgandamizo huo na hivyo kumegeka na kutengeneza tope ambalo ndilo lililoporomoka kufuata mkondo wa mto Jorodom huku likizoa mawe na miti na kuvamia makazi ya binadamu yaliyokuwa pembezoni mwa mto na chini ya mlima Hanang.

“Ifahamike kwamba mlima Hanang umeundwa na miamba laini ya chembechembe za mchanga utokanao na volkano (volcanic sediments,” imamelizia taarifa hiyo wataalamu wa Wizara ya Madini pamoja na Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania, yaani Geological Survey of Tanzania (GST).

Chapisha Maoni

0 Maoni