Naibu Waziri wa Nishati, Mhe. Judith Kapinga ametoa wito kwa
wananchi kulinda miundombinu ya umeme vijijini ili iendelee kuwa na thamani kwa
sasa na vizazi vijavyo.
Mhe. Kapinga ametoa wito huo leo, Tarehe 6 Desemba, 2023
katika Kata ya Makuyuni iliyopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe
Vijijini mkoani Tanga wakati akikagua Mradi wa Kupeleka Umeme Awamu ya Tatu,
Mzungungo wa Pili, unaotekelezwa na mkandarasi, kampuni ya Tontan Ltd chini ya
usimamizi wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
“Ninaendelea kuwaomba, mlinde miundombinu ya miradi hii
kwani miradi hii ni ya thamani kubwa, tuoneshe ushirikiano kwenye utekelezaji
wa miradi hiyo kwani miradi hii haina fidia na inagharamiwa kwa fedha nyingi,
ikiwa na lengo la kupeleka huduma kwa wananchi hivyo niwaombe kutoa ushirikiano
ili miradi isichelewe, kama eneo lako litatakiwa kupita nguzo toa ushirikiano
kwa kuwa umeme unaopita hapo hauna madhara,” ameeleza Mhe. Kapinga.
Aidha, Mhe. Kapinga amebainisha kuwa, Serikali itaendelea
kuleta fedha katika jimbo hilo la Korogwe vijijini na itazidi kusimamia miradi
hiyo ikamilike kwa wakati ili wananchi wote wapate huduma ya umeme.
Pia amesema, Serikali itaendelea kusimamia kwa karibu
wakandarasi wote waliopewa zabuni ya kutekeleza miradi ya kusambaza umeme
vijijini ili kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa
ili iwanufaishe wananchi kama ilivyopangwa.
Mbali na hayo, Mhe. Kapinga amewataka wakandarasi
wanaotekeleza miradi hiyo kutenda haki kwa wananchi kwa kukamilisha miradi hiyo
kwa wakati kwani kulegalega kwao kunakwamisha maendeleo kwa wananchi hao.
Kwa upande wake Msimamizi wa miradi ya REA mkoa wa Tanga
Mhandisi Balisidya Myula amebainisha kuwa Jimbo la Korogwe Vijijini lina Jumla
ya Kata 29, Vijiji 118 na Vitongoji 610 ambapo vijiji 91 sawa na asilimia 77%
vilipatiwa huduma ya umeme kupitia Miradi ya REA III (Mzunguko wa Kwanza na wa
Pili) hivyo vijiji 27 ambavyo havina umeme vinataraji kuunganishwa na huduma ya
umeme kabla ya Mwezi Juni, 2024.
Akizungumzia Mradi wa REA III (Mzunguko wa Pili) katika
Kijiji cha Sharaka, Mhandisi. Myula amesema Mradi huo unatekelezwa kwa gharama
ya shilingi milioni 151.5 na mkandarasi (Kampuni ya Tontan Ltd) umekamilika kwa
asilimia 80 na kazi iliyobaki inatarajiwa kumalizika ifikapo Tarehe 31 Desemba,
2023.
Mhandisi Myula ameitaja Miradi mingine inayotekelezwa katika
Jimbo la Korogwe vijijini kuwa ni pamoja na Mradi wa Kupeleka Umeme kwenye
Migodi Midogo na Maeneo ya Kilimo; Mradi wa Kupeeka Umeme kwenye Vituo vya Afya
na Pampu za Maji na Mradi wa PERI Urban III.
Nae Msimamizi wa Miradi kutoka kampuni ya Tontan Ltd,
Mhandisi, Lomayan Mollel amewaomba radhi wananchi wa kijiji cha kwa
kuchelewesha utekelezaji wa mradi huo na kuahidi kuwa mradi huo utakamilika
ifikapo desemba 31, 2023.
“Ninaomba radhi kwa wananchi kwa kuchelewesha huduma hii ya
kupatikana kwa umeme katika kijiji cha Makuyuni, ninaahidi Mradi huu
utakamilika, ifikapo Desemba 31, 2023 kwani kwa sasa, tupo hatua za mwisho za
ukamilishaji,” ameeleza Mhandisi Mollel.
Serikali kupitia REA inaendelea kutekeleza miradi mbalimbali
ya kusambaza nishati ya umeme vijijini ambapo Wakala umeendelea kutekeleza
Miradi mbalimbali katika Jimbo la Korogwe vijijini, ikiwa na lengo la kuwapa
wananchi huduma bora ya nishati ili kuboresha huduma za kiafya kijamii na
maendeleo ya kiuchumi vijijini.
Na Issa Sabuni na Beatrice Lyimo
0 Maoni