Waliokufa Hanang wafikia 65 na majeruhi sasa ni 117

 

Taarifa ya Serikali ya maendeleo ya hali baada ya maafa maporomoko ya ardhi yaliyotokea Wilayani Hanang mkoani Manyara yaliosababishwa na mvua imeeleza kuwa hadi kufikia leo asubuhi jumla ya vifo vya watu 65 vimethibitishwa.

Taarifa hiyo itatolewa katika Ukumbi wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hanang’ zilizopo hapa Katesh, imeeleza kuwa kati ya waliokufa watu wazima ni 41 (wanaume 15 na wanawake 26), watoto ni 24 (wanaume 10 na wanawake 14).

Miili 65 ilipokelewa na kuhifadhiwa katika Kituo cha Afya Simbay, Kituo cha Afya Magugu, Hospitali ya Dareda, Hospitali ya Mji wa Babati, Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini), na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

Mkurugenzi wa Idara ya Habari (Maelezo) na Msemaji Mkuu wa Serikali amesema katika taarifa hiyo kuwa hadi kufikia leo saa 1:00 asubuhi, jumla ya majeruhi 117 walikuwa wameshapokelewa katika Kituo cha Afya Gendabi, Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini) na Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara.

Kati ya majeruhi hawa 18 hawakuwa na hali nzuri na walihamishiwa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Manyara kwa matibabu zaidi ambapo mmoja (1) kati yao alifariki dunia siku moja baadaye, tarehe 04 Desemba, 2023, saa 4:00 usiku. Majeruhi wengine 17 bado wanaendelea na matibabu hospitali hapo.

Majeruhi wengine 74 ambao hawakupelekwa hospitali ya mkoa bado wanaendelea kupata huduma katika Hospitali ya Wilaya ya Hanang (Tumaini) na Kituo cha Afya Gendabi mjini Katesh. Na majeruhi waliotibiwa na kupata nafuu hatimaye kuruhusiwa kurejea nyumbani ni 25.

Taarifa hiyo imeongeza kuwa jumla kaya 1,150 zenye watu 5,600 zimepoteza makaazi yake katika mji mdogo wa Katesh na vitongoji vya Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Gendabi, Sarijandu, Arukushay na Sebasi.

Serikali inatoa wito kwa kampuni, mashirika, taasisi za umma na binafsi, wadau mbalimbali na wananchi kwa ujumla kujitolea kwa hali na mali ili kuwaisaidia wenzetu waliopatwa na janga hili. Bado tunahitaji vyakula, vifaa, mitambo, madawa na mahitaji mengine.

Kwa misaada ya fedha, Waziri Mkuu ameelekeza, kwamba mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Maafa Na. 6 ya mwaka 2022 na kanuni zake za mwaka 2022, fedha zote zitumwe kwenye akaunti ya Kamati ya Maafa ya Taifa: National Disaster Management Fund Electronic Account 9921151001 kwa kuandika neno MAAFA HANANG. Benki yoyote ndani na nje ya nchi inaweza kupokea fedha kupitia akaunti hii.

Chapisha Maoni

0 Maoni