Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) imeungana na wananchi wa
Mji mdogo wa Katesh Wilayani Hanang, Mkoani Manyara na kupeleka msaada wa dawa
na vifaa tiba vyenye thamani ya TZS. 38 Mil ili kusaidia jitihada za utoaji
huduma katika eneo hilo, ambalo hivi karibuni lilikumbwa na maafa ya mafuriko
yaliyosababisha maporomoko ya udongo kutoka mlima Katesh na kuleta madhara
makubwa ikiwemo vifo, majeruhi, upotevu wa mali na uharibifu wa miundombinu.
Akizungumza kwa Niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa MNH, Mkuu wa
Idara ya Famasi, Mfamasia. Nelson Faustine amesema sambamba na msaada huo,
Hospitali imetuma Msaikolojia Tiba kwenda kuungana na timu za watalam
mbalimbali walioko kule wanaotoa huduma kwa waathirika wa mafuriko hayo.
Hatua hii pia ni kuitikia wito wa Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameagiza kupelekea
watalaam wa saikolojia kuzungumza na wananchi waliopata mfadhaiko kutokana na
tukio hilo ili waweze kurejea katika hali ya kawaida.
Bodi ya Wadhamini, Menejimenti na Wafanyakazi wa Hospitali
ya Taifa Muhimbili wanaendelea kutoa pole kwa wananchi wa Mji mdogo wa Katesh
Wilayani Hanang, Mkoani Manyara kutokana na madhara waliyopata.
0 Maoni