Idadi ya watu waliokufa kwenye maporomoko ya matope ya Mlima
Hanang yaliyotokea wilayani Hanang mkoani Manyara yaliosababishwa na mvua imeongezeka
na kufikia watu 80, huku mwili mmoja wa mwanamke ukipatikana hii leo.
Akiongea na waandishi wa habari leo huko Katesh Msemaji Mkuu
wa Serikali Bw. Mobhare Matinyi ametoa mchanganuo wa waliokufa kuwa watu wazima ni
48 (wanaume 19 na wanawake 29) na watoto ni 32 (wa kiume 15 na wa kike 17).
Matinyi amesema mwili mmoja wa mtoto wa kiume ambao ulikuwa
haujatambuliwa hadi jana sasa umetambuliwa lakini kuna mwili wa mwanamke mmoja
mtu mzima uliopatikana leo ambao bado haujatambuliwa. Hivyo, jumla ya maiti
zilizokwishatambuliwa hadi sasa ni 79.
Maafa ya maporomoko ya matope yaliziathiri kata za mji mdogo
wa Katesh za Jorodom, Ganana, Katesh na Dumbeta pamoja na vijiji vya Sarijandu,
Arukushay na Sebasi vya kata ya Gendabi, vyote kwenye tarafa ya Katesh,
wilayani Hanang, mkoani Manyara.
0 Maoni