Mifugo ipatayo 345 na Trekta moja imekamatwa ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha na askari wa hifadhi hiyo waliokuwa doria wakitekeleza majukumu yao kwa mujibu wa Sheria ya Hifadhi za Taifa Tanzania Sura ya 282 marejeo ya mwaka 2002.
Swala la uingizwaji wa
mifugo na kilimo ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha limekuwa ni tatizo sugu licha
ya wananchi wanaozunguka hifadhi hiyo kupewa elimu inayohusiana na madhara na
kadhia inayoweza kulikumba Taifa kutoka na uharibifu wa ardhi Oevu ya Ihefu
ambayo ni chanzo cha maji yanakwenda kuzalisha umeme katika mabwawa ya
kimkakati nchini.
Kamishna Msaidizi Mwandamizi
wa Uhifadhi Godwell Meng’ataki Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ruaha alisema, mifugo
hiyo 345 imekamatwa na askari wakiwa doria tarehe 13 na 14 Novemba, 2023 zaidi
ya kilometa 100 ndani ya ardhi Oevu. Wafugaji hao wamebuni mbinu ya kuingiza
mifugo usiku wa manane na kuiondoa alfajiri".
Aidha, "Mnamo tarehe
14.11.2023 askari wetu wa Uhifadhi wakiwa doria pia, walifanikiwa kuwakurupua
majangili kadhaa waliokuwa wakilima ndani ya Hifadhi ya Taifa Ruaha kwa kutumia
Trekta aina ya Solanika lenye namba za Usajili T.377 EBA kinyume cha Sheria
zilizoanzisha Hifadhi za Taifa Tanzania".
Kamishna Meing’ataki
aliongeza kuwa baadhi ya majangili hao walikimbia kusikojulika lakini dereva wa
Trekta amekamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria. Pia mifugo hiyo 345
iliyokamatwa na askari hao imefikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Maafisa na askari wa Hifadhi
ya Taifa Ruaha wameendelea kukabiliana na vitendo vya ujangili ndani ya bonde
la Ihefu ili kuhifadhi vyanzo vya maji kwa ajili ya "The Great Ruaha"
na bioanuai zilizomo katika hifadhi hiyo ya pili kwa ukubwa Tanzania kwa ajili
ya maendeleo ya utalii na kuongeza pato kwa Taifa.
Na. Jacob Kasiri - Ruaha.
0 Maoni