WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wathamini wote wawe waadilifu, wenye weledi na wazingatie miiko ya taaluma katika kazi zao za kila siku.
Mhe. Majaliwa amesema kuwa
wathamini ni watu muhimu katika kufanikisha mipango ya maendeleo ya Taifa.
“Mnapaswa kuwa waadilifu na kuzingatia thamani halisi ya ardhi, jengo au
chochote kinachofanyiwa uthamini,” amesema.
Waziri Mkuu Mhe. Majaliwa amesema
hayo jana wakati akifungua Mkutano Mkuu wa Nne wa Mwaka wa Wathamini
unaofanyika kwa siku mbili katika Kituo cha Mikutano cha Jakaya Kikwete, jijini
Dodoma.
“Kazi ya uthamini si ya
wababaishaji au vishoka, hivyo basi kila mthamini hana budi kuthamini na
kuheshimu taaluma yake.”
Mhe. Majaliwa amesisitiza
kuwa: “Wapo baadhi ya wathamini ambao si waadilifu kwa kushirikiana na
watendaji wengine hutoa makadirio ambayo hayawiani na thamani halisi. Vitendo
hivyo husababisha kupoteza mapato ya Serikali lakini pia kuwanyima haki wale
wanaostahili kupata haki.”
Aidha, Mheshimiwa Majaliwa
amewataka watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi hususani
wathamini washirikiane na sekta binafsi kufanya kazi za uthamini. “Tumieni
fursa ya uwepo wa wathamini binafsi ili kutoa huduma bora na ya haraka hapa
nchini, kufanya hivyo mtakuwa mnatekeleza maagizo ya Rais Dkt. Samia Suluhu
Hassan ya ushirikishaji wa sekta binafsi kwa maendeleo ya Taifa.”
Katika hatua nyingine,
Mheshimiwa Majaliwa amewataka wathamini hao watumie mkutano huo kufanya
majadiliano ya kina kuhusu masuala ya taratibu za utwaaji ardhi na sheria zake,
ukokotozi wa fidia katika maeneo ya madini, viwango vya thamani ya ardhi na
mazao, changamoto za kisera za utwaaji ardhi pamoja na kupata suluhu ya
malalamiko ya wananchi.
Naye, Naibu Waziri wa Ardhi,
Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Geoffrey Pinda amesema kuwa uthamini wa fidia ni
ufunguo wa maendeleo na mabadiliko chanya ya kiuchumi kwa kuwa unawezesha
wawekezaji kupata ardhi na kuwekeza mitaji yao.
Amesema kuwa Wizara kwa
kushirikiana na Bodi ya Usajili wa Wathamini nchini imejipanga kuhakikisha
shughuli zote za uthamini zinaboreshwa. “Wizara itasimamia upatikanaji wa
huduma hii kwa wananchi kwa wakati, kutatua kero mbalimbali za wananchi katika
eneo hili la fidia na kuwezesha Bodi kuwachukulia hatua kali wale wote
wanaohujumu shughuli za uthamini nchini.”
Amesema kuwa uthamini
hufanyika na kuwezesha upatikanaji wa ardhi itakayotumika kwa ajili ya matumizi
ya umma, kuweka miundombinu ya msingi, huduma za jamii, viwanda na kupanga
makazi.
CHANZO: Ofisi ya Waziri Mkuu
0 Maoni