Kamati ya Kudumu ya Bunge ya
Viwanda, Biashara, Kilimo na Mifugo imetoa pongenzi kwa Wakala wa Usajili wa
Biashara na Leseni (BRELA) kutokana na mabadiliko mbalimbali ya utendaji kazi
yanayofanyika katika Taasisi hiyo.
Pongezi hizo zimetolewa jana
na Mwenyekiti Kamati hiyo Mhe. Deo Mwanyika (Mb)wakati wa Semina Maalumu
iliyoandaliwa na BRELA jijini Dodoma kuwaelimisha wajumbe wa Kamati hiyo
majukumu yanayofanywa na Taasisi hiyo.
Bw. Mwanyika amesema changamoto
zilizokuwepo awali za kiutendaji kwa sasa hazipo na matokeo yake BRELA
inaendelea kufanya kazi kwa weledi na uadilifu.
Kwa upande wake Naibu Waziri
wa Viwanda na Biashara Mhe. Exaud Kigahe (Mb), akimwakilisha Waziri wa Wizara
hiyo amesema, elimu zaidi inapaswa kutolewa ili kuwa na uelewa mpana kuhusu
majukumu yanayofanywa na BRELA.
“Kama mnavyoona kuna baadhi
ya mambo mliyoyaeleza hapa Waheshimiwa Wabunge ndiyo wanayasikia hivyo semina
hizi ni muhimu kufanyika mara kwa mara pamoja na kuwa na muda wa kutosha,”
ameeleza Mhe. Kigahe.
Awali Afisa Mtendaji Mkuu wa
BRELA aliwaeleza wajumbe Kamati hiyo kuwa BRELA inaendelea kufanya maboresho
mbalimbali ya kimifumo lengo likiwa ni kuhakikisha kuwa wadau wanapata huduma
za BRELA kwa urahisi zaidi.
Amewahakikishia kuwa taarifa
za wadau wote waliofanya sajili mbalimbali BRELA ambazo zinafanyika kwa njia ya
mtandao zipo salama na Taasisi imekuwa ikishirikiana na Mamlaka ya Serikali
Mtandao (eGA) kuhakikisha kuwa mfumo unakuwa salama wakati wote.
Kwa upande wake Mjumbe wa
Kamati Mhe. Prof. Sospeter Muhongo (Mb) alitaka kufahamu kama BRELA ina mpango
wowote wa kuwasaidia wabunifu waliojisajili BRELA kwa kuwatafutia masoko ya
Bunifu zao.
Akitoa ufafanuzi Msajili
Msaidizi Mkuu wa BRELA Bw. Seka Kasera amesema Wizara ya Viwanda na Biashara
ilianza mchakato wa kuwa na Sera ya Taifa ya Miliki Ubunifu ambapo maoni ya
wadau yameshachukuliwa na sasa Sera hiyo iko hatua ya mwisho na itakapokamilika
itawezesha kuwapatia masoko wabunifu mbalimbali ambao wamesajili bunifu zao
BRELA.
Bw, Seka amesema kuwa Sheria
iliyopo sasa inaiwezesha BRELA kutoa linzi pekee kwa Bunifu mbalimbali.
“Sheria ya Miliki Ubunifu
itakapofanyiwa marekebisho haitaishia kuweka linzi pekee bali itahakikisha kuwa
bunifu hizo zinaingia sokoni ili wabunifu waweze kunufaika na bunifu zao”,
amefafanua Bw, Seka.
Naye Mjumbe wa Kamati hiyo
Mhe. Abdul-Aziz Abood alitaka kufahamu BRELA inashugulikiaje suala la ufanano
wa majina ya Kampuni na ya Biashara wadau wanapopeleka maombi ya majina
yanayofanana.
Akifafanua kuhusu hoja hiyo Msajili Msaidizi wa BRELA Bi. Leticia Zavu amesema vigezo vinavyotumika katika usajili wa Kampuni na Majina ya Biashara ni kutokuwa na ufanano wa matamshi na maandishi hivyo aliyesajiliwa awali ndiye hulindwa na kuendelea kutumia jina husika.
Katika semina hiyo BRELA iliwasilisha mada kuhusu utekelezaji wa Sheria ya Usajili ya Kampuni na Majina ya Biashara, Sheria ya Leseni za Biashara na Viwanda pamoja na Sheria ya Usajili wa Alama za Biashara na Huduma.
0 Maoni