Rais wa Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ameruhusu kuanzishwa kwa mchakato wa
kurejesha kumbukumbu na vifaa vya jadi na utamaduni vinavyohusiana na historia
ya Tanzania akiwemo mjusi mkubwa aina ya Dinosaur aliyeko nchini Ujerumani
ambaye ni kivutio kikubwa cha utalii nchini humo.
Hayo yamesemwa bungeni na
Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Angellah Kairuki (Mb) alipokuwa akitoa
taarifa kuhusu hoja ya Mhe. Riziki Lulida aliyetaka kujua lini Serikali ya
Tanzania itanufaika na mapato yatokanayo na mjusi aina ya Dinosaur ambapo
Ujerumani inapokea mapato ya takriban dola bilioni 3.8 kama faida inayotokana
na maonyesho ya mjusi huyo aliyeko katika Makumbusho ya Ujerumani.
“Nikuhakikishie tayari kama
Serikali kupitia mazungumzo ya Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyoyafanya
na Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeir tunayo kamati ya kiserikali yenye
taasisi zaidi ya nane ambayo itasimamia suala hili na baadae tutaendelea na
majadiliano ambayo mheshimiwa Rais ametoa baraka zake” Mhe. Kairuki
amesisitiza.
Hatua hiyo ya mazungumzo
baina ya nchi hizo mbili inakuja ikiwa
takribani wiki mbili sasa tangu Rais wa Ujerumani, Frank-Walter Steinmeir
alipofanya ziara ya kikazi nchini Tanzania.
Amefafanua kuwa Serikali iko
katika taratibu za kidiplomasia kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano
wa Afrika Mashariki ili mazungumzo rasmi yaanze kuhusiana na 'artifacts' zote
na vifaa vingine ambavyo ni kwa ajili ya kumbukumbu ya Tanzania ikiwemo mjusi
pamoja na mengineyo.
Kwa upande wake Mhe. Lulida
alifafanua kuwa kutokana mapato inayopata Ujerumani kwa kumuonyesha mjusi huyo,
Serikali ya Tanzania inaweza kupata gawio ili iweze kuliendeleza eneo la
Tendaguru Mkoani Lindi ambako mjusi huyo alikochukuliwa.
Na Happiness Shayo -Dodoma
0 Maoni