Mwenyekiti wa Chama cha ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman,
ambaye pia alikuwa mgombea urais wa Zanzibar kupitia chama hicho, ameanza ziara
maalum ya siku nne kisiwani Pemba yenye lengo la kuimarisha mshikamano wa wanachama
na kufufua ari ya kisiasa ndani ya chama hicho.
Ziara hii, ambayo ni ya kwanza tangu kumalizika kwa uchaguzi
mkuu wa Oktoba 29, imeanza kwa hamasa kubwa, huku maelfu ya wafuasi na
wanachama wa ACT Wazalendo wakijitokeza kwa wingi kumpokea kiongozi wao katika
ofisi za mratibu wa chama eneo la Gombani, wilaya ya Chake Chake.
Akihutubia wananchi katika mkutano huo, Othman Masoud
alisema kuwa huu ni wakati wa Wazanzibari kusimama imara kwa umoja na
mshikamano ili kulinda amani, utu na heshima ya Zanzibar.
Ameeleza kuwa chama chake kitaendelea kusimama kidete katika
kudai uchaguzi huru, haki na ushirikishwaji wa kweli wa wananchi katika maamuzi
yanayohusu mustakabali wa taifa.
Aliongeza kuwa, “Tunataka Zanzibar yenye uwazi, usawa na
uadilifu. Tunataka demokrasia inayojengwa juu ya misingi ya heshima na haki kwa
wote. Huu ndio urithi tunaoutaka kwa vizazi vijavyo.”
Othman pia alitumia fursa hiyo kuwashukuru wanachama wa ACT
Wazalendo kwa kuendelea kuwa na imani na chama, akiwataka kuendeleza juhudi za
kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa umoja, maendeleo na uadilifu wa kisiasa.
Ziara ya Othman Masoud inatarajiwa kuendelea katika mikoa
yote minne ya kichama kisiwani Pemba, ambapo atakutana na viongozi, wanachama
na wananchi kwa lengo la kusikiliza changamoto zao na kujadili mustakabali wa
Zanzibar katika siasa za sasa.


0 Maoni